Home » » PIRAMIDI YA AFYA: UGONJWA WA MAFINDOFINDO KWA WATOTO

PIRAMIDI YA AFYA: UGONJWA WA MAFINDOFINDO KWA WATOTO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Kumekuwa na uelewa  mdogo wa suala la vidonda vya koo maarufu kama mafindofindo katika jamii zetu.
Watu wengi wamekuwa wakiamini ugonjwa huu unasababishwa na utumiaji wa vitu vya baridi kama kama vile barafu na icecream.
Dhana hii potofu imesababisha wazazi wengi kuwapiga marufuku watoto wao kutumia wakidhani ndiyo chanzo kikuu. Leo nitaelezea ugonjwa huo wa mafindofindo ama kwa kitaalamu tonsillitis.
Mafindofindo ni mjibizo wa tezi iitwayo tonsil, ambayo husaidiana na tezi nyingine katika mwili kupambana na vimelea mbalimbali vya magonjwa kwa kutengeneza askari mwili.
Tezi hizi ziko mbili na zinapatikana pande zote mbili nyuma ya koo. Zina rangi ya pinki na mara zinapovimba baada ya maambukizi hubadilika na kuwa nyekundu.
Mafindofindo ni ugonjwa ambao huambukizwa kwa njia ya hewa, ambapo vimelea vya magonjwa kama vile bakteria na virusi huenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali.
Mojawapo ni kwa kupiga chafya, kukohoa, kugusa zana yenye vimelea na kugusisha mdomoni au masikioni.
Ugonjwa huu huwapata watoto zaidi ingawa huweza kuathiri pia watu wa rika nyingine.
Dalili kuu ya ugonjwa huu ni vidonda kooni. Mara nyingi mgonjwa hulalamika kuwa na vidonda kooni ambavyo huambatana na maumivu  makali wakati wa kumeza chakula.
Dalili nyingine zinazoambatana na vidonda kooni ni uvimbe wa tezi unaodhihirika  mbele ya shingo, homa kali, kichwa kuuma, mafua, harufu mbaya kinywani, kufifia au kupotea kwa sauti na mwili kuchoka. Vidonda kooni ambavyo huambatana na dalili nyingine kama vile mafua, kupiga chafya na kikohozi mara nyingi husababishwa na virusi.
Kwa sababu hiyo, matibabu ya dawa katika hali hiyo si ya lazima kwa sababu mwili unaweza kupambana katika kuondoa vijidudu hivyo.
Endapo vidonda vya koo havitaambatana na dalili yoyote kama nilizozitaja, moja kwa moja kinachodhaniwa ni maambukizi ya bakteria.

Njia mbadala za kutibu ugonjwa huu ni pamoja na kupumzika, kusukutua kinywa kwa kutumia maji vuguvugu yenye chumvi na kunywa maji mengi.
Dawa za maumivu na homa hutolewa na wakati mwingine dawa za vijaviuasumu (antibiotics) huweza kutumika iwapo maambukizi ni ya bakteria.
Endapo ugonjwa hautapatiwa tiba ya haraka, madhara mbalimbali huweza kujitokeza kama vile  homa ya rheumatic, magonjwa ya sikio, figo, tezi nyingine pia katika mwili zaweza kuathiriwa pia kwa kutengeneza usaha.
Mwendelezo wa maambukizi ya tezi hizi za koo, huweza kusababisha mafindofindo sugu. Hii ni kutokana na kuendelea kuzaliana kwa bakteria ambao hutengeneza vifuko vidogo kwenye tezi hizo.
Ndani ya vifuko hivi hutengenezwa mawe madogo yaliyo na mchanganyiko wa salfa ambayo huleta harufu mbaya ya kinywa. Mara nyingi mafindofindo sugu hutibiwa kwa njia ya upasuaji. Hii huamriwa na daktari endapo maambukizi hayo yatakuwa yameendelea kumsumbua mgonjwa kwa kipindi kirefu. Upasuaji utamsaidia mgonjwa kuepuka madhara kwenye mifumo mingine.
Ili kuepuka kupata maambukizi katika mfumo wa hewa ni vyema kuzingatia usafi wa mwili na mikono.
Epuka sehemu ambazo utakaa muda mrefu ambazo zinavihatarishi kama vile msongamano wa watu na vumbi.
 Chanzo mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa