Home » » NI MAJANGA TENA POLISI

NI MAJANGA TENA POLISI

   Wengine hoi kwa kipigo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda.
Jeshi la Polisi limekubwa na dhahama nyingine baada ya  askari wake wawili wa mkoani Tabora, kupewa kipigo kwa madai ya kusababisha kifo cha kijana mmoja wa mjini humo.
 Tukio hilo lilitokea juzi sambamba na tukio la kuuawa kwa askari wawili wa kituo polisi cha Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.
 Aidha, Jeshi la Polisi limeungana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuwasaka watu waliovamia Kituo cha Polisi Ikwiriri wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani na kuwaua askari hao na kupora silaha mbalimbali zikiwamo bunduki na risasi.
 Katika tukio la Tabora, kijana huyo anadaiwa kufa wakati akifukuzwa na askari hao wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora kwa lengo la kutaka kumtia mbaroni kwa tuhuma za  kushiriki mchezo wa kamari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, akizungumza na NIPASHE alisema tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu  saa 10.30 jioni katika mtaa wa Kadinya kata ya Ng’ambo.
Kamanda Kaganda aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  PC Yohana na MW Daniel Isonda na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitete  kutokana na kujeruhiwa kwa kipigo na wananchi.
Alisema wananchi walianza kuwashambulia askari hao walipotaka kuwakamata vijana watatu waliokuwa wakicheza kamari kijiweni katika eneo la Ng’ambo mjini Tabora.
Vijana hao baada ya kubaini wanataka kukamatwa na polisi walianza kukimbia na bahati mbaya mmoja wao alitumbukia ndani ya dimbwi la maji na kuzama.
Kaganda alisema kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Edwin Kefa (19), baada ya kutumbukia katika dimbwi hilo,  alishindwa kuogelea na hivyo askari waliokuwa wakimfukuza walimuokoa akiwa katika hali mbaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Kitete, lakini alifariki  wakati akipatiwa matibabu.
Alisema pamoja na askari hao kushambuliwa, Jeshi hilo litaendelea kufanya msako mkali ili kuvunja vijiwe vyote vya wacheza kamari, wavuta bangi na wanaotumia dawa za kulevya mkoani Tabora.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wananchi walichukua uamuzi wa kuwashambulia askari hao baada ya kuona wakimpiga  kijana aliyepoteza maisha kabla ya kufikwa na mauti.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kitete, Dk. Yusuph Bwire, alisema hali za askari hao zinaendelea vizuri na kwamba  Isonda alijeruhiwa begani na kichwani.
Dk. Bwire alisema Yohana alijeruhiwa kichwani na kwamba aliruhisiwa jana asubuhi  baada ya hali yake kuwa nzuri.
JWTZ YAJITIOSA RUFIJI
Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliokiteka na kukivamia kituo cha polisi Ikwiriri na kuwaua askari wawili na kuiba silaha.
Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, akizungumza katika mahojiano na Redio One katika kipindi cha Kumepambazuka, alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanatiwa mbaroni.
Kamishna Chagonja alisema hadi kufikia jana jioni hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa na wamebaini kuwa bomu lililorushwa katika kituo hicho halikuwa moja bali yalikuwa mengi.
“Uvamizi ulikuwa mkubwa na inaonekana waliofanya tukio hilo  walikuwa si chini ya 15 na baada ya kufanya tukio hilo waliondoka kwa kutumia Noah,” alisema.
Alisema mabaki ya bomu lililorushwa yamepekwa kwa wataalam kubaini ni bomu la aina gani.
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, alisema tukio la kuvamiwa kituo hicho lilitokea saa 8:00 usiku.
Kamanda Matei alitaja askari waliouawa kuwa ni PC Judith Timoth na  Koplo Edga Mlinga ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani na kwamba miili ya askari  imehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri.
Alisema baada ya kukivamia kituo hicho waliiba bunduki aina ya SMG mbili, SAR mbili, Shotgun moja, risasi zaidi ya 60 na bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
 Matei alisema baadaye walilipua bomu kituoni hapo ambalo liliharibu gari lenye namba PT 1965 linalotumiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo hicho (OCCID) kisha kutokomea kusikojulikana.
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jeshi hilo lina idara nyingi, hivyo taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kushirikiana katika uchunguzi wa tukio hilo zinaweza kuwa za kweli.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. KUELEKEA UCHAGUZI 2015: JE UNAPENDA NANI AWE KIONGOZI WAKO? JAZA FOMU HII FUPI HAPA docs.google.com docs.google.com

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa