‘Toeni ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili mauaji yakomeshwe’
MBUNGE wa Kaliua mkoani Tabora, Magdalena Sakaya (Cuf), amewaomba
wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kukomesha mauaji
yanayoendelea wilayani humo.
Sakaya alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Usangi, kata ya Igwisi, wilayani Kaliua.
Alisema mauaji hayo yamekuwa yakimnyima usingizi kwani yanakithiri
kila uchao hali ambayo inahitaji kuangaliwa kwa ukaribu na serikali.
Aidha, alisema amekuwa akipokea taarifa za mara kwa mara za watu
kuuana kinyama kwa sababu mbalimbali na kueleza kuwa, wananchi wanapaswa
kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola na serikali kuongeza ulinzi kwa
wananchi wake.
Sakaya alisema baadhi ya sababu za mauaji hayo alielezwa kuwa ni
visasi, kufumaniwa, mali, mashamba, vurugu za wafugaji na baadhi ya
askari wa Maliasili.
Aidha, alisema hata katika vilabu vya pombe, minada, wakulima
waliouza mazao na tumbaku na hata katika mchezo wa Pool, mauaji
yametokea.
Alitolea mfano wa mauaji ya hivi karibuni ya kijana kumpiga mwenziwe
na fimbo ya mchezo huo (pool table) na kusababisha kifo chake. Sakaya
alidai pia kuwa, vipo vitisho vinatolewa kwa viongozi wa kisiasa na
kueleza kuwa mambo hayo hayapaswi kufumbiwa macho na wenye dhamana ya
usalama wa raia na mali zao.
Alisema ana ushahidi wa kiongozi mmoja wa ngazi ya Kata ya Igwisi na
kundi lake kumtishia kumuua Mwenyekiti wa Kitongoji cha Upele, Madiseni
Selina.
Alisema kiongozi yupo kwa ajili ya wananchi wote bila kujali itikadi
cha vyama na hapaswi kuwa sababu ya vitisho kwa namna yoyote na kwa mtu
yeyote.
Pia, alikemea baadhi ya watu katika kikosi cha ulinzi cha Sungusungu
katika maeneo ya Kaliua kujichukulia sheria mkononi ya kukamata watu
ovyo na wakati mwingine kuwajeruhi kwani inaondoa sifa ya Sungusungu
kama jeshi la kulinda amani vijijini.
Siku chache zilizopita, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri,
alimuaagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Khamis Issa, kukomesha mauaji
ya kinyama yanayoendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment