Home » » MFUGAJI AMSHAMBULIA MWANANCHI NA KUMJERUHI

MFUGAJI AMSHAMBULIA MWANANCHI NA KUMJERUHI

Hastin Liumba, Uyui
MKAZI wa Kijiji cha Lunguya, Kata ya Upuge, wilayani Uyui, mkoani Tabora, Moshi Shaban Chimagula (54) amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa na mfugaji aliyetajwa kwa jina la Jilala Peter baada ya kushambuliwa na fimbo sehemu za mwili wake akizuiwa kulisha mifugo yake katika shamba hilo.

Chimagula alisema amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo tumboni, mbavu na kifuani na alipatiwa PF 3 na kwenda kutibiwa Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Kitete.

Chimagula alifafanua kuwa tukio hilo lilimtokea majira ya saa 11:00 jioni, Agosti 3, Mwaka huu, akiwa nyumbani kwake ambapo alipata taarifa kuwa bustanini kwake kuna mfugaji aliyetajwa kwa jina la Jilala analisha mifugo yake na ndipo alipoamua kwenda kumwondoa.

Alisema alipofika na kujaribu kumwondoa alianza kushambuliwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo tumboni, mbavuni na kichwani hali iliyosababisha  kuendelea kupata matibabu hadi sasa huku mbavu na kifua bado vikiwa na matatizo.

Mkazi huyo alifafanua zaidi kuwa alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Lunguya aliyemtaja kwa jina la Peter Mahanga, ambaye alimpatia barua ya kwenda kutibiwa, barua ambayo iliandikwa Agosti 4, mwaka huu.

Alisema baada ya kupewa barua hiyo alikwenda kituo cha afya cha Kata ya Upuge, lakini alijibiwa aende Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Kitete, ndipo alipofunga safari na kuanza matibabu yake hadi sasa na baada ya picha ya X-Ray aligundulika ana hitilafu kwenye mbavu zake na kifua.

Aidha kabla ya kwenda hospitali alipitia polisi na kufungua kesi ya shambulio iliyopewa namba,UY/RB/594/2012, na alipewa PF 3 iliyojazwa na askari WP 9019 PC Johari, lakini hadi sasa mfugaji huyo hajakamatwa na yeye bado ana maumivu makali.

"Kinachonishangaza ni polisi kushindwa kumkamata mtuhumiwa huku mimi nikiwa natishiwa maisha na mfugaji huyo kuwa nitauawa, na mwenyekiti wa kijiji hicho anayo taarifa lakini wamekaa kimya hadi sasa.

Alisema hadi sasa maisha yake yapo hatarini kwani anatishiwa kuuawa na mfugaji huyo na zaidi ni kwamba shamba lake ambalo analima nyanya, matango, matikiti maji, kabichi, mchicha na spinachi, sehemu kadhaa imechomwa moto.

"Nimefanya juhudi kuuelezea uongozi wa kijiji, wakiwemo polisi lakini hadi sasa ni kimya na mimi naendelea na kutishiwa maisha, kazi sasa katika shamba langu nimesimama kutokana na maumivu ambayo yanaendelea." alisema.

Alisema kila anapofuatilia kesi yake anapigwa danadana na zaidi hata mwenyekiti wa Kijiji cha Lunguya, Paulo Mahanga alimtamkia OCD wa Wilaya ya Uyui kuwa anashindwa kumkamata mtuhumiwa kwani ni tishio sana pale kijijini.

Chimaguli ameiomba Serikali ya Mkoa wa Tabora kumsaidia kwani vitisho dhidi yake vinaendelea na amekuwa akiishi kwa hofu  kila anapotaka kuchukua hatua zaidi na hana msaada wowote kwani hata uongozi wa kijiji unamwogopa mfugaji huyo.

Gazeti hili lilimtafuta mwenyekiti wa Kijiji cha Lunguya,Paulo Mahanga ambaye alikiri kuwepo kwa tukio hilo na yeye alishatoa barua kwa mhanga kwenda kutibiwa na zaidi yeye yupo tayari kutoa ushahidi mahakamani endapo kesi hiyo itahitajika kufanya hivyo.

Hata hivyo mwenyekiti huyo alikana kuwa mfugaji huyo anatikisa kijiji hicho na anaogopwa hata kufunguliwa kesi ya jinai na kusisitiza kuwa polisi wanayo taarifa juu ya tukio hilo la mwananchi wake kuumizwa.

Aidha alikiri ni kweli bustani na shamba la mwananchi Chimaguli lililishiwa mifugo na  Jilala ikiwemo sehemu kadhaa kuchomwa moto, ambapo alisema yeye ni mwenyekiti tu hawezi kumkamata mfugaji huyo.

Naye  Jilala Peter alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu tuhuma hizo alikata simu na kuizima, akiwa malishoni na jitihada za kumpata zilipofanyika haikuweza kujulikana aliko.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora, Anton Rutta alipotafutwa na gazeti hili alisema suala hilo halijamfikia mezani kwake na kuahidi kulifuatilia ili kama kuna ukweli hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake kukomesha tabia hiyo.


Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa