TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha
mahakamani Ofisa Usafirishaji wa Kampuni ya Athwal Transport &
Timber LTD , Godfrey Tarimo, kwa mashitaka ya kutoa rushwa kwa mtumishi
wa kampuni hiyo akiri kosa la wizi.
Tarimo alipandishwa kizimbani jana, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mkoa wa Tabora Jackton Rushwela .
Wakili wa Takukuru, Simon Mashingia alidai Tarimo alitenda kosa hilo Februari 13 mwaka huu katika Gereza la Uyui mjini hapa.
Wakili Mashingia alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa akiwa ni Ofisa
Usafirishaji wa ATT alitoa rushwa ya Sh 400,000 kwa Said Hamis ambaye
alikuwa utingo wa gari katika kampuni ya ATT.
Akifafanua katika mashitaka hayo, wakili Mashingia alidai kuwa Tarimo
akiwa kama wakala wa kampuni alitoa fedha hizo kama kishawishi
kitakacho mfanya Hamisi akiri kosa la wizi katika kesi ya jinai namba
13/2015 iliyokuwa inamkabili.
Ilidaiwa kwamba, Hamisi baada ya kupokea fedha hizo alipofika
mahakamani alikiri kosa ambapo Hakimu Rushwela alimpa adhabu ya kifungo
cha miaka mitano jela. Mwendesha mashitaka alidai, uchunguzi umebaini
kuwa Tarimo alipoteza tumbaku iliyokuwa inasafirishwa na magari ya
kampuni ya ATT.
Alidai kwamba, ili kampuni hiyo isionekane ina sura mbaya katika
biashara, walimbambikia kesi utingo huyo na kumshawishi akubali kuwa
ndiye aliiba ili baadaye waweze kumsaidia atoke lakini alihukumiwa
kifungo.
0 comments:
Post a Comment