Hatima
ya makada watano wa Chadema, wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, inatarajiwa kujulikana leo, wakati
mahakama hiyo itakapotoa uamuzi kuhusiana na kesi hiyopamoja na mambo
mengine, uhalali wa mashtaka yanayowakabili.
Makada
hao wa Chadema, Henry John Kilewo, ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya
Kinondoni, Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Daniel, Seif
Magesa Kabuta, walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa
mashtaka mawili, moja la ugaidi na lingine la jinai.
Katika
shtaka la kwanza wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi,
wakidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha huko Igunga, Tabora, na
la pili wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu wakidaiwa
kumdhuru Tesha kwa kumwagia tindikali.
Walidaiwa
kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa
Jimbo la Igunga.Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mawakili wao, Peter
Kibatala na Profesa Abdallah Safari walipambana kuwanusuru na mashtaka
hayo.
Mawakili
hao walihoji uhalali wa mashtaka hayo,wakidai kuwa hakuna vigezo vya
kutosha kuonyesha kuwa kuna ugaidi, huku pia wakihoji utaratibu wa
kuwafungulia mashtaka katika mahakama hiyo badala ya kule
walikokamatiwa.
Hivyo
waliiomba Mahakama hiyo ama iwafutie mashtaka hayo au iamuru kila
mshtakiwa arudishwe na kushtakiwa katika mahakama za mahali
walikokamatiwa.
Upande wa
mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Juma Masanja akisaidiana na
Wakili wa Serikali, Idelfonce Mukandara, walidai mashtaka hayo ni
halali.
Baada ya
kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Joctan
Rushwera aliahirisha kesi hiyo na kupanga kutoa uamuzi leo.
Hakimu
Rushwera aliamuru washtakiwa wote wapelekwe mahabusu wakisubiri uamuzi
wa kesi yao leo, kwa kuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.
CHANZO JUMA MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment