AFISA Tarafa ya Kaliua Wilaya ya Kaliua mkoani
Tabora, Josephat Brown anatuhumiwa kumbaka mama lishe na kumsababishia maumivu
makali na kisha kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo limetokea Agosti 29 mwaka huu, saa tano
usiku nyumbani kwa afisa tarafa huyo baada ya kumrubuni mama huyo (jina) mwenye
miaka (38) katika baa iitwayo Leaders akitaka ampelekee nyama ya kuku ana
wageni.
Kwa mujibu wa maelezo ya mama huyo katika kituo cha
polisi wilaya ya Kaliua, siku hiyo wakati akiuza nyama ya kuku wa kukaanga
kwenye baa, mtuhumiwa alimuomba ampelekee kitoweo hicho nyumbani.
Alisema kuwa baada ya kukubali waliongozana naye
hadi nyumbani kwa afisa tarafa huyo na baada ya kufika alimuamru amsokotee
bangi iliyokuwa mezani huku akiwa amemshikia kisu akimtisha kumuua.
Baada kusokotewa bangi hiyo, afisa huyo aliivuta
huku akimpulizia moshi mama lishe usoni na baada ya kumaliza alimshikia kisu
tena na kumuamuru avue nguo wafanye mapenzi.
Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa mama huyo aligoma
kufanya tendo la ndoa, ndipo afisa tarafa alipomuingilia kwa nguvu hali ambayo
ilizusha tafrani kidogo.
Baada ya kubakwa, mama huyo alipata upenyo na
kukimbilia kwa wasamaria wema ambapo alisaidiwa kufika kituo cha polisi na
kuandikisha maelezo ya tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Saveli Maketa alikiri
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa afisa tarafa huyo hadi sasa hajulikani
alipo.
“Tukio hilo kweli lipo na limeripotiwa kituo cha
polisi na linachunguzwa lakini mtuhumiwa ametoweka karibu wiki nzima sasa
hajafika kazini bila ya taarifa zozote na ofisi yake hadi sasa imefungwa,”
alisema.
Aliongeza kuwa jalada la kesi hiyo
Kumb/RB/1058/2013 limefunguliwa polisi na maelezo ya kina juu ya tukio hilo
yameshafikishwa kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, Peter Ouma.
Maketa alisema kuwa afisa tarafa huyo alikuwa
ofisini kwake na kwamba aliwahi kumuonya juu ya matumizi ya bangi na dawa za
kulevya ambazo alikuwa akitumia.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Peter Ouma,
alisema suala la afisa tarafa kutuhumiwa kumbaka mama lishe bado halijamfikia
mezani kwake, hivyo hawezi kulizungumzia hadi hapo atakapopata taarifa sahihi
toka OCD wilaya ya Kaliua.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment