Home » » UJENZI DARAJA LA MBUTU, SERIKALI YAOKOA SHILINGI BILIONI 18

UJENZI DARAJA LA MBUTU, SERIKALI YAOKOA SHILINGI BILIONI 18


Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga Bw. Elibariki Kingu (kulia), wakikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mbutu linalojengwa katika wilaya ya Igunga mkoani wa Tabora.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mbele) akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mbutu linalojengwa katika wilaya ya Igunga mkoani wa Tabora.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mbele) akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mbutu linalojengwa katika wilaya ya Igunga mkoani wa Tabora.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mbele) akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mbutu linalojengwa katika wilaya ya Igunga mkoani wa Tabora. 

******
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Serikali imeweza kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 18 kwa kutumia makandarasi wa kizalendo kujenga Daraja la Mbutu. Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Waziri Magufuli amebainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo umegharimu kiasi cha Shilingi bilioni 12 badala ya Shilingi bilioni 30 endapo lingejengwa na Makandarasi wa nje.

Daraja la Mbutu pamoja na tuta la barabara lenye urefu wa kilometa 3 linajengwa na muungano wa Makandarasi wa Kizalendo 13 unaojulikana kama Mbutu Bridge Joint Venture chini ya usimamizi wa muungano wa Wahandisi Washauri wawili (2) unaojulikana kama PIDAEL Joint Venture. Makandarasi hao wanafanyakazi ya kusanifu na kujenga kwa wakati mmoja kwa gharama hiyo ya Shilingi bilioni 12 ambapo fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzani.

Mkataba wa ujenzi wa Daraja la Mbutu ulisainiwa Aprili, 2012 na umepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa 2013.

“Nimeridhishawa na kasi ya ujenzi wa daraja hili na nimeona tayari mmefikia karibu asilimia 80, hii ni kazi nzuri inayostahili kupongezwa kwani mmeanza kudhihirisha uwezo wenu kama Makandarasi wazalendo” alisisitiza Waziri Magufuli na kuwataka Makandarasi hao kuhakikisha kuwa wanaukamilisha mradi huo kwa muda na viwango vilivyopangwa.

Mheshimiwa Magufuli pia amewataka wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha kwamba wanalitumia daraja hilo vizuri kwani hiyo ni fursa nyingine ya kuwaletea maendeleo. Hata hivyo aliwatahadharisha wasafirishaji watakaotumia daraja hilo kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kutozidisha uzito uliowekwa kisheria.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga Bw. Elibariki Kingu, kwa upande wake alimshukuru Waziri Magufuli na kwamba mambo aliyojionea na kutoa maelekezo yatasaidia kukamilika kwa daraja hili kwa wakati na hivyo kuleta faraja kubwa kwa wananchi wengi wanaoitumia barabara hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Magufuli amewahakikishia wananchi wa Igunga kuwa Serikali itajenga barabara ya lami kutoka mji wa Igunga hadi Mbutu. Azma hiyo imetokana na maombi ya wananchi wa maeneo hayo waliyoyatoa katika nyakati tofauti na pia kwa kuzingatia adha iliyokuwa ikiwakabili kiasi cha kufikia baadhi ya wananchi na mifugo yao kupoteza maisha kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano ya barabara na daraja la uhakika katika eneo hilo hasa nyakati za mvua.
Kwa Hisani ya Michuzi Blog

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa