Home » » MADIWANI CCM BADO WAMNG`ANG`ANIA MEYA TABORA.‏

MADIWANI CCM BADO WAMNG`ANG`ANIA MEYA TABORA.‏


Na Hastin Liumba,Tabora
 

 
SAKATA la madiwani halmashauri ya manispaa Tabora kutaka kumg`oa
mstahiki meya wa manispaa hiyo Ghulam Hussein dewji Remtullah
limechukua sura mpya baada ya madiwani hao kumuandikia barua
mkurugenzi kuitisha kikao cha baraza cha dharura.
 
Madiwani hao wameandika barua hiyo mwezi disemba 10 mwaka huu yenye
kichwa cha habari kisemacho ‘ombi la kuitishwa mkutano maalumu wa
halmashauri kwa madhumuni ya kumuondoa madaraka mstahiki meya Ghulam
Hussein Dewji Remtullah kwa kutokuwa na imani naye’.
 
Kwa mujibu wa barua hiyo yenye orodha ya madiwani waliojiorodhesha
majina na sahihi zao kutaka kumuondoa meya wao,imesema kutokana na
kanuni za kudumu za halmashauri ya manispaa Tabora, kanuni namba 80
kifungu a,c na d wako sahihi kufanya hilo.
 
“Sisi madiwani tupatao 28….tukiwa na akili zetu timamu na bila
kushawishiwa na mtu yoyote tumeweka sahihi zetu hapo nyuma kutaka
kumuondoa mstahiki meya kwa kushindwa kazi na kutokuwa na imani
naye.”ilisema sehemu ya barua hiyo.
 
Aidha barua hiyo ya madiwani hao inaeleza zaidi kuwa lengo la kuomba
mkutano maalumu wa madiwani ni meya huyo kutumia nafasi yake
vibaya,kushindwa kazi na mwenendo mbaya wa kutosimamia na kuheshimu
maazimio ya mikutano.
 
Barua hiyo ilifafanua kuwa chini ya uongozi wa mstahiki meya huyo
ameshindwa kusimamia mapato na matumizi kwa kutofikia malengo katika
kujiendesha kiasi cha kuwepo ubadhirifu mkubwa na kupelekea kupata
hati chafu mwaka wa fedha wa 2011/212.
 
Aidha tuhuma nyingine ni mstahiki meya na kamati yake ya fedha,utawala
na uongozi kutembelea miradi ya maendeleo na kushindwa kutoa taarifa
ya ukaguzi kwenye vikao vya halmashauri toka amekabidhiwa kiti hicho.
 
Meya huyo anatuhumiwa kufumbia macho ubadhirifu wa jengo la OPD kata
ya Itetemia lililojengwa kwa sh milioni 100 badala ya sh milioni 40
kama alivyoelezwa mkuu wa mkoa wa Tabora Fatma Mwassa na kuwepo
ubadhirifu wa ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari ya kata ya
Ndevelwa.
 
Tuhuma nyingine ni safari ya Marekeani ya mstahiki meya akiongozana na
mtalaam Deo Msilu mwezi april 2011 ikiwa ni ziara ya urafiki wa
Millenium City ambapo safari hiyo iligharimu sh milioni 17 fedha
ambazo walitakiwa kupata kibali cha halmashuri alkini hawakufanya
hivyo.
 
Aidha barua hiyo imeanisha aliyekuwa mkurugenzi wakati huo Fanuel
Senge naye alisafiri kwenda nchini Ethiopia na alitumia fedha za
halmashauri bila kufuata utaratibu lakini fedha hizo alirejesha na hii
inamlazimu mstahiki meya naye arejeshe fedha hizo lakini amekaidi.
 
Katika tuhuma nyingine madiwani hao waliorodhesha jinsi meya huyo
alivyojilimbikizia viwanja na kuvitaja ni Plot namba 100 area G 4070
mtrs PB chenye jina Marial Hilal, Plot namba area 158 G 6980 mtrs
Ghulamhussein Remtullah, Plot namba 99 area F 3331 mtrs Dewji
Ghulamhussein.
 
Barua hiyo ilitaja viwanja vingine kuwa ni Plot namba 206 area C 2252
mtrs Gulan F Gulan,Plot namba 637 Block D 3.11 Heka 8.5 Gulam H
Remtullah na hali hiyo inapelekea kuwa meya huyo amekiuka maadili ya
uongozi na kutumia cheo chake kujilimbikizia mali.
 
Aidha madiwani hao walisema tuhuma nyingine ni mstahiki meya kutumia
nafasi yake kuwagwa madiwani na kutengeneza chuki kiasi cha wengine
kujiuzulu nafasi zao za ujumbe wa kamati ndogo.
 
Gazeti hili lilimtafuta mstahiki meya wa manispaa Tabora Ghulamhussein
Remtullah kujibu tuhuma hizo lakini alikana na kudai ni chuki za watu,
huku mkurugenzi wa manispaa huyo Alfred Luanda naye alikiri kupokea
barua hiyo ya madiwani hao.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa