Home » » WAKULIMA NA WAFUGAJI WATAKIWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA‏

WAKULIMA NA WAFUGAJI WATAKIWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA‏


 
Na Hastin Liumba, Sikonge
 
SERIKALI imewataka wakulima na wafugaji  kujiepusha na vitendo vya
kuomba au kupokea rushwa katika utekelezaji wa shughuli zao za kila
siku.
 
Kupokea ama kutoa rushwa kunawafanya kuwepo mianya wa kuibiwa na
kuminywa haki zao za msingi, uonevu, kuongeza uhasama na unyanyaswaji.
 
Mkuu wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Hanifa Selengu alisema hayo
wakati akiongea na wakulima wa vijiji vya Mitowo na Kidete  kata ya
Tutuo ikiwa ni ziara maalumu ya kutembelea, kuhamasisha na kuhimiza
shughuli za kimaendeleo.
 
Alisema katika maeneo mengi rushwa imekithiri lakini inachangiwa na
wakulima na wafugaji wenyewe kwa lengo la kutaka kujipatia mali katika
njia isiyo halali huku wakificha uharifu wao kupitia migongo ya
viongozi wa vijiji, vitongoji na kata husika.
 
‘Wafugaji walio wengi wamekuwa jeuri, wanawapa rushwa viongozi wa
vitongoji, vijiji na kata ili wasiwachukulie hatua au wasikamate
mifugo yao hali ambayo inazidisha uhasama kati yao na wakulima, acheni
tabia hiyo mara moja’, alisema mkuu wa wilaya.
 
Aidha ili kumaliza vitendo hivyo amewataka wakulima na wafugaji
kupatana na kushirikiana ili waendelee kuwa kitu kimoja kama
ilivyokuwa hapo awali kwani wote ni jamii moja, pia ameagiza watendaji
wa vijiji na kata kuwatengea maeneo maalumu ili kuepusha migongano na
uhasama kati yao.
 
‘Tumekubalina kimsingi wafugaji watengewe eneo lao la kufugia na
wakulima wapate eneo la mashamba na nimeagiza viongozi wa vitongoji na
vijiji hivyo watengeneze njia au barabara maalumu za kupitisha mifugo
ili isiwe inapita kwenye mashamba ya wakulima, ‘aliongeza.
 
Ili kumaliza kero mbalimbali zinazowakabili wakulima hasa wa zao la
tumbaku na wafugaji hao, DC ameshauri viongozi wa vitongoji,vijiji na
kata hizo wawe wanafanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi ili
kusikiliza kero zilizopo na kuzifanyia kazi.
 
Aidha alibainisha kuwa wamekubaliana kupunguza idadi ya mifugo ambapo
kila kaya inatakiwa kuwa na mifugo isiyozidi 20, ile itakayozidi iuzwe
ili fedha hizo zitumike kufanya mambo mengine ya kimaendeleo mfano
kujenga maduka, nyumba nzuri za kuishi na nyumba za kulala wageni.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa