Home » » DC Sikonge akabidhi madawati 214 kwa msingi

DC Sikonge akabidhi madawati 214 kwa msingi

 Kilio cha muda mrefu cha uhaba wa madawati kwa shule za msingi katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora kimeanza kupungua baada ya halmashauri ya wilaya hiyo kuanza jitihada za makusudi kutengeneza madawati kwa ajili ya shule hizo.
Wilaya hiyo yenye shule za msingi 87 zikiwa na jumla ya wanafunzi 32,862 inakabiliwa na upungufu wa madawati 6,008 kati ya 14,477 yanayohitajika na imedhamiria kumaliza kero hiyo ili kuwaondolea adha wanafunzi wanaosoma katika shule hizo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi madawati 214 kwa afisa elimu shule za msingi wilayani humo juzi, mkuu wa wilaya hiyo Hanifa Selengu alisema kuwa wameazimia kutumia asilimia 60 ya mapato ya ndani kutengeneza madawati ili kumaliza uhaba uliopo.
Alisema mkakati mwingine utakaosaidia kumaliza kero hiyo ni kuwabana wafanya biashara wanaovuna mbao kuchangia asilimia 50 ya mapato yatokanayo na mazao hayo ya misitu kwa ajili ya madawati.
" M p a k a s a s a tumetengeneza madawati 450, leo hii nakabidhi 214 na yaliyobaki yatakuwa tayari mwezi ujao (Januari), tumedhamiria kutengeneza madawati 1,000 kila mwaka ili kumaliza upungufu huo," amebainisha.
Aidha alisema wataongeza hamasa kwa wananchi na kamati za shule ili nao wajitolee kutengeneza madawati kwa ajili ya shule zilizoko katika maeneo yao mkakati ambao utasaidia kudumish
 dhana ya ushirikishwaji wananchi katika shughuli za kimaendeleo.
Aidha amewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo yenye misitu kuilinda na kuitunza kwani umuhimu wake ni mkubwa sana katika jamii hasa katika utengenezaji wa madawati hayo na shughuli zingine za kiuchumi kama vile ufugaji nyuki na nyinginezo.
Amebainisha kuwa upungufu wa madawati katika wilaya hiyo unaathiri kwa kiasi kikubwa utoaji elimu katika shule hizo kwa kuwa unachochea vitendo vya utoro kwa baadhi ya wanafunzi jambo ambalo linaathiri matokeo katika mitihani yao ya mwisho.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo Gervas Magashe, amesema kuwa wameweka utaratibu wa kutoza asilimia 25 katika uwindaji wa kitalii unaofanyika wilayani humo na kiasi hicho mbali na matumizi mengineyo pia kitasaidia kutengeneza madawati.
Aidha alisema misitu ya hifadhi wilayani humo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uvamizi unaofanywa na wakulima, wafugaji na wavuna mbao wasiokuwa na vibali, hali ambayo imewalazimu kuweka doria na kuongeza faini kwa wote wanaokamatwa

Chanzo;Majirra

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa