TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeokoa zaidi
ya sh milioni 100 zilizokuwa zimeibwa na watumishi wa halmashauri za
wilaya mkoani Tabora kati ya Januari na Novemba mwaka huu.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kuhusu hali ya vitendo vya
rushwa, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Fidelis Kalungura, alisema
wameweza kuokoa sh milioni 107.3 ambazo watumishi wa idara mbalimbali
katika halmashauri walitaka kuiba kwa kudanganya malipo yake.
Kalungura alisema baada ya TAKUKURU kupokea malalamiko na kero
mbalimbali toka kwa wananchi, ilifuatilia na kubaini ubadhirifu huo na
watuhumiwa wake walikubali kulipa madeni yao na malalamiko yao
yalirudishwa kwa waajiri kwa hatua nyingine za kinidhamu.
Alibainisha kuwa watumishi wengi wa umma hasa walio katika serikali
za mitaa ndio wamelalamikiwa kwa wingi mwaka huu kuhusiana na vitendo
vya kuomba na kupokea rushwa.
Pia alisema taasisi yake ilipokea malalamiko mengi na kero za watumishi kutoka idara za utawala, afya na misitu.
Alisema taasisi yake itawashughulikia watuhumiwa wote bila kujali
cheo na nafasi ya mtu katika jamii, na kuwataka watumishi kuwa
waaminifu na kufanya kazi zao kwa uadilifu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment