Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kutokana na kuondolewa kwa Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Shaaban
Salum na Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Issa bin Simba, baadhi ya
Waislamu wamedai kitendo hicho hakivumiliki.
Sheikh Salum alivuliwa uongozi na kupewa barua
iliyosainiwa na Sheikh Simba inayoeleza kuwa ameshindwa kutekeleza
matakwa ya kufuta usajili wa Msikiti wa Ijumaa kutoka kwa Wakala wa
Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) baada ya kupewa miezi mitatu kufanya
hivyo.
Akizungumza kwenye Msikiti wa Ijumaa baada ya
Swala ya Alasiri, Sheikh Salum aliwaeleza waumini kuwa amevuliwa uongozi
kutokana na mkakati wake wa kuwaendeleza Waislamu.
“Nimesimama kuwaeleza kuwa nimekumbwa na kadhia
leo (jana), pengine nitabaki kuwa imamu kwani nimevuliwa uongozi siyo
tena Sheikh wa Mkoa kutokana na mkakati na mpangokazi wangu wa maendeleo
ambao umesababisha kuvuliwa madaraka,” alisema Sheikh Salum.
Alisema alikuwa na mipango ya kujenga maduka
kuzunguka msikiti na kwamba ana uhakika wameweza kupata Sh10 milioni
ambazo zitatumika kwa manufaa ya Waislamu.
Sheikh Salum aliwalaumu watu wasiowatakia mema ambao alidai wamejaa husuda, huku akiwaita waongo na wanafiki duniani na ahera.
Akitoa msimamo wa Waislamu wanaoswali msikiti
hapo, msemaji wa msikiti huo, Abuu Bakari alisema hawatambui kuvuliwa
uongozi kwa Sheikh Salum na kwamba wanaendela kumtambua.
“Tunatoa taarifa kwa Mufti, Waislamu hususani wa
Msikiti wa Ijumaa kuwa tunamtambua Sheikh Shaaban Salum kama Sheikh wa
Mkoa. Tunamtambua hivyo na tunamwagiza mufti alete mtu atueleze sababu
za kumtoa kwenye wadhifa wake,” alisema.
Bakari aliitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora,
Seleiman Kumchaya kutoa taarifa za kuvurugwa kwa waumini wa Kiislamu,
vinginevyo yatakayotokea asije akalaumu watu wa Tabora. Baadhi ya
waumini waliunga mkono tamko hilo na kudai wataendelea kumtambua kama
kiongozi wao na kwamba Simba amevunja Katiba. ya Bakwata na kutaka
aondolewe kwenye wadhifa wake huku wakisisitiza Sheikh Salum
alichaguliwa na Waislamu ambao ndiyo wanaopaswa kuelezwa makosa
aliyotenda ili wamhukumu siyo kuondolewa kinyemela.
“Kama mufti ameona Sheikh Salum amefanya makosa
kwa nini hakuchagua mtu miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Ulamaa, badala
yake amechagua mtu kutoka nje ya baraza hilo?” alihoji Kansa Mbarouk.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment