Saa tano asubuhi katika kliniki ya Kirando iliyopo mkoani Rukwa,
mama mmoja mjamzito anasubiri huduma katika ofisi ya mhudumu wa afya.
Amekuja kliniki kuangalia maendeleo ya ujauzito
wake. Safari hii kaja peke yake lakini anasema siku za nyuma alishawahi
kwenda hapo na mumewe.
Kwa kliniki ya Kirando kuwa na wanaume
wanaowasindikiza wenza wao sio jambo geni, ndiyo maana hatua chache
kutoka katika ofisi aliyomo mjamzito huyu, wanaume kadhaa wanaonekana
wakichanganyika na wanawake waliokuja kliniki.
Wanaume hawa wengi wao wakiwa vijana, wamekuja kliniki kuwasindikiza wenza wao kujua maendeleo ya mimba na hata afya za
Inawezekana kwa baadhi ya watu ikawa kioja kusikia
kuwa mume naye anakwenda kliniki sambamba na mkewe, lakini wanaume
wengi wamebadili mtazamo kuhusu masuala yanayohusu afya ya uzazi.
Zamani iliaminika kwa wengi kuwa wajibu wa
mwanaume ni kutungisha mimba, lakini kazi ya kuilea, kuzaa, afya na
malezi ya mtoto ni majukumu ya mwanamke pekee.
Hata hivyo, kupitia elimu kwa umma na hamasa kwa
jamii kupitia juhudi za Serikali na wadau wengine, ushiriki wa wanaume
katika masuala ya afya ya uzazi umeongezeka.
Wanaume Rukwa
Mkoani Rukwa wanaume wengi wamebadilika kimtazamo
na kitabia hasa baada ya wengi kufikiwa na mafunzo ya mradi wa ushiriki
wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi (TMEP), unaofadhiliwa na
Chama cha elimu ya afya ya uzazi cha Sweden (RFSU).
Meneja Mradi, Dk Cuthbert Maendaenda, anasema
mradi pamoja na mengineyo unalenga kuhakikisha kuwa wanaume na wanawake
wana haki sawa katika masuala ya uhusiano na uzazi.
‘’Ili uzazi utoke lazima wawili hawa washiriki
pamoja lakini ikaonekana wajibu wa mwanaume unakwisha baada ya
kusababisha mke kupata mimba, mengineyo kama kupima ujauzito, kumpeleka
mtoto kliniki, kuzuia maambukizo ya mtoto kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto vinabaki kwa manamke,’’ anasema.
Anaongeza: ‘’Mradi wa TMEP unasisitiza wanaume
kujua kuwa nao ni wateja wa masuala ya afya ya uzazi. Ili kuwepo na
uhusiano mzuri tunataka wanaume wawasaidie wenza wao.’’
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kirando, Dk Anastazi Kisinda
anasema tangu jamii ifikiwe na mradi wa TMEP, ushiriki wa wanaume
kuwasindikiza wenza wao kliniki kwa ajili ya kupata huduma za afya
umekua kwa kiasi kikubwa.
“Siku za nyuma haikuonekana kama kitu cha kawaida,
lakini sasa inaonekana kuwa kitu cha kawaida. Zamani hakuna mwanamume
aliyekuja lakini sasa kwa siku hatuwezi kukosa wanaume 20 au 25
kutegemea ukubwa wa kliniki ya siku hiyo,’’ anaeleza.
Anasema ili kuhamasisha wanaume kuhudhuria kliniki, walianzisha utaratibu wa kuwapa kipaumbele wanawake wanaokuja na waume zao.
“ Awali changamoto tuliyoipata wanaume walifikiri
kuja ni kupoteza muda, tukawapa ari wanawake waliokuja na wenza wao kwa
kuwahudumia haraka kuliko wenzao, ‘’anasema.
Marieta Hamisi ni mwanamke aliyeamua kufunga
kizazi. Anasema hakupata tabu kumshawishi mume wake haja ya kufanya
hivyo baada ya kuwa na idadi ya kutosha ya watoto wanaoweza kuwahudumia.
“Nilipomweleza mume wangu hakunibishia, alinielewa
hivyo tukafunga kizazi. Hapa kwetu wanaume wengi wanakwenda kliniki na
wenza wao,’’ anasema Marieta ambaye ni mkazi wa kijiji cha Matai
wilayani Kalambo.
Ukiondoa wanaume kwenda kliniki, mkazi wa Manispaa
ya Sumbawanga, Joel Charanda, anasema haoni aibu kumsaidia katika
majukumu ya nyumbani.
“Najua majukumu ya baba nikiwa nyumbani, nakwenda
hata sokoni, nikirudi nabeba mtoto, wenzangu wananishangaa ukiangalia
sisi bado ni vijana.Lazima nimsaidie mke wangu kwa sababu sijamuoa kuja
kuwa mtumwa,’’ anasema.
Anaongeza: “Mwanaume hana budi kutambua kuwa yeye na mke wake wana majukumu sawa katika kuleta maendeleo.’’
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment