Katika kile kinachoonekana waigizaji wa kike kutaka kukuza
tasnia ya uigizaji kwa kuvuka mipaka ya nchi, mwigizaji Irene Uwoya
amesema kuwa anataka atambulike nje ya nchi kuliko ndani.
Akiweka hoja yake sawa, mwanadada huyo anayedaiwa
kuendelea kuwa na mvuto katika tasnia ya filamu alisema anajua kuwa siyo
jambo rahisi kufanya vizuri nje ya nchi, lakini huko ndiko anakotaka
kufika, hivyo inyeshe mvua au liwake jua, atajitahidi kuhakikisha kwamba
ndoto zake zinatimia.
Uwoya alisema kuwa alijaribu kutengeneza mtandao
wa kazi na wasanii wa nje wakati anatayarisha filamu ya ‘Kisoda’ ambayo
picha zake zilipigwa nchini Afrika Kusini na Uturuki. Alifafanua kama
wakati mwingine siyo lazima kusafiri, kuna wakati wasanii wa nje
wanaweza kuja Tanzania kikazi, ujio wao ni nafasi ya pekee kwao, au kwa
kufanya nao kazi hapahapa, ama kuchukua mawasiliano na kuwafuata baadaye
kwa ajili ya kufanya nao kazi.
“Tena nawaambia wale wote wenye nafasi au
wanaofahamiana na watu wanaopenda kwa dhati kufanya kazi na waigizaji wa
Tanzania, wasikose kuwaambia hata mimi napenda na ninaweza kufanya
hivyo, ”alisema Uwoya.
Mwigizaji huyo alifafanua kuwa njia pekee ya
kutangaza kazi za ndani Kimataifa ni kufanya kazi na waigizaji wa nchi
nyingine ambao watakuwa na hamu ya kukufuatilia na kufuatilia kazi zetu
nyingine pia. Aliongeza kuwa kwenye muziki angalau kuna mwanga, lakini
kwenye uigizaji bado juhudi inahitajika kwani baada ya kufariki dunia
kwa mwigizaji Steven Kanumba, mbio za kujitangaza kama zimefifia.
Kauli hiyo ya Uwoya imekuja wakati waigizaji
kadhaa wakionyesha nia kama yake akiwamo Wastara anayenadi filamu mpya
ya ‘Mateso wanayopata Watanzania nje ya nchi’ na mwigizaji anayedaiwa
kuwa na nguvu ya kukubalika kwenye jamii Wema Sepetu akiwa amerudi juzi
kutoka nchini Ghana ambako alikwenda kupiga picha za filamu yake iitwayo
‘After Death’.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment