BALOZI wa Tanzania nchini China, Abdulrahman Shimbo ameshauri mitaala ya elimu iingize masuala yanayowaunganisha Watanzania ili kuvisaidia vizazi vya sasa na vijavyo kuilinda nchi.
Miongoni mwa mambo aliyoshauri yapewe nafasi kubwa katika mitaala ni masuala ya kihistoria yanayobeba hatma ya nchi kama Mapinduzi ya Zanzibar, Uhuru na Muungano na kutaka masuala hayo, yatengewe muda zaidi mashuleni na kuzungumzwa pia kila wakati katika maisha ya kila siku.
Ameshauri pia kuwa nchi ielekeze nguvu kubwa katika kuhakikisha mipango ya uchumi iliyopo na itakayowekwa, inalenga kumkomboa mwananchi wa kawaida dhidi ya umasikini kwani ni njia pekee itakayomfanya ajithamini na kuithamini nchi yake.
Balozi Shimbo aliyasema hayo juzi mjini hapa katika mjadala maalumu wa kumbukumbu ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar uliofanyika Ubalozini.
Mjadala huo uliandaliwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania Beijing (TZ-SUB). Akijibu maswali ya washiriki wa mjadala waliotaka kufahamu nini kifanyike kulinda umoja wa Kitaifa dhidi ya mwelekeo hasi wa kusahau mambo ya msingi yanayowaunganisha Watanzania, Balozi Shimbo alisema mtu yeyote atakayepuuza historia ya nchi, ataiingiza nchi kwenye matatizo.
“Mitaala yetu itazame historia na utamaduni wetu, utamaduni wetu unaharibiwa kwa kuiga mambo ya kigeni hivyo tunasahau tulipotoka na hatujui tunapokwenda, Ulaya wanafanya haya, masomo yao yana misingi hiyo,†alisema Balozi Shimbo.
Akifafanua kuhusu tunu za Taifa, Balozi Shimbo alisema Katiba Iliyopendekezwa imeweka Muungano kama Tunu, na kusema kama Katiba ikipitishwa, itasaidia umoja wa nchi kuimarika vizazi na vizazi.
Chanzo: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment