Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Serikali imefanikiwa kumaliza sintofahamu ilikuwepo baina ya wakulima na
wanunuzi wa tumbaku mkoani Tabora juu ya uwepo wa tani 3,700 zilizokosa soko.
Tani 3,700 zilikuwa zimekosa wanunuzi kwa sababu hazikuwa na mkataba
kati ya wakulima na wanunuzi na hivyo kuhitaji utatuzi wa haraka wa Serikali
ili kuinusuru tumbaku hiyo.
“Tumefanikiwa kuongea nao na tutauza zile tani 3,700 kwa wanunuzi,”
alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuamsha shangwe ukumbi mzima.
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo jana jioni (Jumatano, Agosti 9, 2017) wakati
akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi
wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa
Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Aliwashukuru wanunuzi kwa kukubali kumaliza tatizo hilo kwani litaleta
ari mpya kwa wakulima na kuwafanya wajipange vizuri kwa msimu ujao. “Makampuni
ya ununuzi yatapita kwenye maeneo yenu, WETCU watafuatilia na tumekubaliana nao
kuwa tutafanya kazi pamoja,” alisema Waziri Mkuu.
Kufuatia sintofahamu hiyo, wiki iliyopita, wakazi wa mkoa huo
waliomuomba Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aingile kati ili
kuwanusuru na adha ya zao hilo kukosa soko. Naye akawaahidi wananchi hao kwamba
suala hilo atalikamilisha Waziri Mkuu.
Mapema, Mkuu
wa Mkoa wa Tabora, Bw. Aggrey Mwanri
wakati akiwasilisha muhtasari wa taarifa ya mkoa huo alisema katika masoko ya
tumbaku yanayoendelea, kuna tatizo la tumbaku kukosa wanunuzi kwani hapakuwa na mkataba kati ya
wakulima na wanunuzi.
“Tumbaku inayofikia kilo milioni 3.7 kwa sehemu kubwa ililimwa kwa
ufadhili wa WETCU Ltd, kwa fedha
ambazo zilikuwa ziende APEX. WETCU walinunua pembejeo na kuwapa wakulima
waliokuwa chini ya vyama sinzia, na sasa haina wanunuzi. Tunaomba ulisemee hilo
ili tupate ufumbuzi wa suala hili,” alisema.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni mbunge wa Urambo,
Mheshimiwa Margareth Sitta aliiomba Serikali ikubali kuliangalia suala hilo la
tani za ziada 3,700 kwani wakulima wamejaza tumbaku majumbani mwao na kwenye
maghala.
“Wakulima wetu wanahitaji kuuza hii tumbaku ili wapate fedha za kuanzia
msimu ujao wa kilimo. Lakini pia tunaomba liangaliwe suala la upangaji madaraja
ya tumbaku, wasaidiwe kukabili bei isiyotabirika na kutatua ukosefu wa soko la
uhakika,” alisema Mama Sitta.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.
0 comments:
Post a Comment