Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Godfrey Robert Malema
Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Mohammed Bashe anapenda kuwataarifu umma ya kuwa tayari serikali imetoa fedha kiasi cha Shilingi Milioni Mia Mbili (Tzs 200,000,000) maalum kwa ajili ya kutatua matatizo au kero za maji na miundombinu ya maji ndani ya Jimbo la Nzega Mjini.
Kupatikana kwa fedha hizi ni matokeo ya Mhe. Hussein Bashe kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu wakati wa ziara ya kikazi ya Rais mkoani kwetu.
Ili kuhakikisha tunafikia malengo yaliyokusudiwa; Usimamizi wa fedha hizi hautafata taratibu za tenda ila utafuata utaratibu wa kuwa na timu ya pamoja itakayojumuisha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi, Ofisi ya Mbunge, Mamlaka ya Maji, Madiwani wa Kata ya Nzega Mjini Magharibi, Nzega Mjini Mashariki na Wenyeviti wa Serikali ya Mtaa katika maeneo ambayo yatahusika na ukarabati huu mkubwa.
Aidha; Matumizi ya Fedha hizi yatajumuisha Usafishaji na Ukarabati wa Bwawa la Uchama; Ukarabati wa Miundombinu ya Maji ili kusaidia maji kuweza kufika maeneo ya mbali; Ujenzi wa Maghati Matano (5) kutoka Nyasa Mahakamani hadi Stendi Mpya; jambo hili litafanikisha ujenzi wa mtandao mpya wa maji wenye urefu wa zaidi ya mita 200 kupitia mtaa wa Uswilu.
Hivyo; Ofisi ya Mbunge inawataka madiwani wote kushirikiana na Wenyeviti wa serikali za Mitaa kuweza kubaini na kupendekeza maeneo sahihi ya ujenzi wa Maghati haya mapya.
Kipekee kabisa, Mheshimiwa Hussein Bashe anapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa namna anavyoendelea kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Nzega Mjini katika kutatua kero mbalimbali ikiwemo kero na kilio cha muda mrefu juu ya Ukosefu wa Maji.
Na mpaka sasa tayari Rais anakua ametimiza ahadi yake ya kutupatia Tzs 400,000,000 ambazo nilimuomba nyakati tofauti ili kutatua changamoto kubwa za shida ya maji jimboni.
Kwa upande mwingine Mbunge anapenda kuwashukuru Waziri wa Maji Mhe. Gerson Lwenge na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo pamoja na watumishi wote wa Wizara hii kwa namna ambavyo wamekua wakishirikiana nasi katika kusaidia kupunguza matatizo ya maji ndani ya Jimbo la Nzega Mjini huku tukisubiria kukamilika kwa Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria.
Mwisho, Ofisi ya Mbunge inapenda kusisitiza ya kuwa ni wajibu wetu wote kuhakikisha tunalinda vyanzo vyetu vya maji na kutoshiriki kwa namna yeyote katika kuharibu miundombinu ya maji ndani ya Jimbo la Nzega Mjini na mahali popote nchini ili kuvilinda na kuviendeleza vyanzo vilivyopo kwa matumizi endelevu ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo.
0 comments:
Post a Comment