Imeandikwa na Lucas Raphael, Igunga
SERIKALI imesema haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria
madiwani, watakaobainika kuleta uvunjifu wa amani katika kata zao na
halmashauri kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Tabora,
Richard Lugomela (pichani) kwenye kikao cha baraza la madiwani
kilichofanyika mjinji hapa. Lugomela alisema madiwani wa Igunga
wameshindwa kutatua kero zinazowakabili wananchi waliowachagua na badala
yake wameamua kuendeleza migogoro ya kutokuelewana wao kwa wao huku
wakijua kufanya hivyo ni makosa kisheria.
Alisema serikali Mkoa wa Tabora pamoja na wilaya zake, wamejipanga
kikamilifu kuhakikisha wananchi wake pamoja na mali zao wanaishi kwa
amani na usalama pasipo kuingiziwa migogoro na madiwani wao. Alibainisha
kuwa diwani atakayebainika kuweka makundi ya kukwamisha juhudi za
serikali za kuwatumikia wananchi na kuendelea kuleta uvunjifu wa amani,
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na kuwataka madiwani
kuacha kuleta migogoro ya kufarakana kwa maslahi binafsi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Igunga, Godslove Kawishe akizungumza kwa
niaba ya mkuu wa wilaya, John Mwaipopo, aliwataka madiwani kwa
kushirikiana na wenyeviti wa vitongoji na vijiji pamoja na watendaji wa
vijiji kata kutatua kero za wananchi kwa wakati.
Aliwaagiza viongozi hao kusimamia kilimo pindi mvua zitakapoanza
kunyesha, ambapo kila kaya inatakiwa kulima hekari moja ya zao la
chakula ili kukabiliana na janga la njaa. Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Revocatus Kuuli alisema migogoro ya
madiwani waliyonayo, yeye na watumishi wenzake haiwahusu, kwani wao
wanaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na ndiyo maana mapato ya
halmashauri yanaendelea kupanda hadi sasa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment