Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na. Tiganya Vincent - RS-Tabora
Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka katika Manispaa ya Tabora inahitaji jumla ya
shilingi bilioni 15 kwa ajili ya hatua za awali za ujenzi wa mtandao wa
kuondoa maji taka katika maeneo mbalimbali mjini humo.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA, Bwire Mkama
wakati wa uzinduzi wa Malipo kabla ya matumizi ya maji ili kukabiliana
na wadaiwa sugu na wateja ambao upenda kutumia maji bila kulipia huduma
hiyo kwa wakati.
Alisema
kuwa lengo ni kutaka kuwa na miundo mbinu itakayosaidia kuondoa maji
taka katika majumba ya watu na mitaa kwa ajili ya kupeleka sehemu ambayo
yatawekwa pamoja ili kuiepushia jamii na maradhi yanaweza kusababishwa
na kuzagaa kwa maji hayo.
Bwire alisema kuwa Bodi ya TUWASA iliona umuhimu kwa kuanza mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya shughuli hiyo.
Alisema
kuwa hivi sasa wameshaandika andiko la uwekezaji katika mtandao wa maji
taka na kulipeleka Wizarani kwa ajili ya kutafuta fedha za kutekeleza
mradi huo.
Bwire
alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo mapema kwa sababu upatikanaji
wa maji safi na salama unapoongezeka katika miji ndivyo maji taka nayo
yanavyoongezeka.
Alimuomba
Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusaidia kusukuma andiko lao ili fedha ya
utekelezaji wa mradi huo iweze kupatikana na kazi ianze mara moja.
Alisema
kuwa hivi sasa TUWASA ina jumla ya kilometa 20 tu za mtandao wa maji
taka katikati ya mji wa Tabora ambapo ni asilimia 6 tu ya wakazi wa
Manispaa ya Tabora ndio wameunganishwa katika huduma hiyo.
Aidha
alisema kuwa hivi sasa wanashirikiana na Manispaa ya Tabora ili
kuanisha maeneo ambayo wanaweza kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji taka.
Kwa mujibu wa Bwire, mabwawa yaliyopo hivi sasa hajatoshi kutokan na ongezeko kubwa la uzalishaji wa maji taka.
Akijibu
hoja hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alikubali kushirikiana
na TUWASA katika kuhakikisha andiko hilo linafanikiwa na mradi unaanza
ili kuboresha huduma hiyo na kuepusha jamii na magonjwa.
0 comments:
Post a Comment