Home » » UCHELEWESHWAJI MRADI WA KUKU WAWAPONZA MAOFISA WILAYANI UYUI

UCHELEWESHWAJI MRADI WA KUKU WAWAPONZA MAOFISA WILAYANI UYUI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri 

Na. Tiganya Vincent – RS Tabora
 
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amemtaka Katibu Tawala mkoa huo kuuandikia uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kuwachukulia hatua wajumbe wa timu ya mradi wa Miombo Wilayani Uyui kwa sababu za kushindwa kufanya kazi na kuchelewa kuanza kwa mradi wa ufugaji kuku wenye thamani shilingi milioni tano. 
 
Mwanri alitoa agizo hilo jana wakati alipotembea Halmashauri hiyo kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Miombo ambayo ni pamoja na ufugaji nyuki, kuku, samaki, mbuzi, utengezaji wa mkaa mbadala na mingine mingi.
 
Alisema kuwa haiweziekani fedha ziingie kwenye Akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Tabora toka mwezi Julai hadi hivi sasa hazijaelekezwa katika mradi uliokusudiwa wa uanzishaji wa kikundi cha ufugaji wa kuku kwenye vijiji husika.
 
Mwanri alisema kuwa Mradi huo uliokuwa utekelezwa katika vijiji vya Inonelwa, Ibiri na Msimba ungekuwa umeanza kutekelezwa mara baada ya fedha zilizopingia miezi mitatu iliyopita, hivi sasa wananchi wangekuwa wanaendelea na uzalishaji lakini wao wamezikalia tu.
 
“Muda wa ngonjera umekwisha …ukifanya kosa mimi nakushughulikia pale pale ili waje wanaokutetea nao niwashughulike…haiwezekana tukaendelea kufanyakazi kwa mazoea fedha zinakuja, hazipelekwi kwenye miradi iliyokusudiwa kwa sababu ya uzembe wa wachache” alieleza Mwanri.
 
Wajumbe ambao amegizwa wachukuliwe hatua ni wale walioko katika timu ya mradi wa miombo wilayani hapo ambao ni pamoja na Mratibu wa Mradi Wilaya Kaliua, Afisa Mifugo, Afisa Kilimo, Afisa Ushirika na Afisa Nyuki.
 
Kwa upande wa Mratibu wa Miombo Kitaifa Yobu Kiungo alisema kuwa athari za ucheleweshaji wa mradi wowote unaweza kusababisha mradi huo kupelekwa katika maeneo mengine ambayo yatakuwa tayari kuuchangamkia.
 
Alisema kuwa athari nyingine kuwa endapo miradi iliyopangwa kutekelezwa katika eneo husika katika kipindi fulani isipofanyika kwa zaidi ya asilimia 80 inathiri hata maeneo meninge ya mkoa husika.
 
Kiungo alitoa wito kwa Wakurugenzi Watendaji wa Manispaa ya Tabora, Wilaya ya Tabora, Urambo na Kaliua ambapo ndipo miradi hiyo inatekelezwa kuunga mkono juhudi zinafanyika ili iweze kukamilika kwa wakati na iweze kuwa na manufaa kwa wakazi wa eneo husika.
 
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Hadija Makuwani alisema kuwa alilazimika kuzuia fedha baada ya kutoridhishwa na maandalizi ya mabanda ya kuku katika vijiji hivyo.
 
Alisema kuwa aliamua kuchukua taadhari ili fedha hizo zisije zikapotea kwa kupeleka katika eneo ambao wanakijiji hawajiandaa na mradi.
 
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amemwagiza Mkaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa kutoka ofisini kwake Hamis Mjanja kupitia miradi yote ya Miombo iliyopo katika Wilaya ya Uyui ili kuona kama thamani yake inalingana na fedha zilizotolewa na mradi.
 
Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kutaka kujiridhisha kama kweli kinachoenda kwa wananchi ndio kile kilichoandikwa katika vitabu na siovinginevyo.
MWISHO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa