Mbunge
wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameonya kuwa endapo chama hicho hakitataka
kuambiwa ukweli na kukosolewa, utakuwa mwanzo wa kuanguka kwake.
Nape
aliyewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, amesema
endapo CCM itaua utamaduni wa kukosoana kupitia vikao itapoteza
mwelekeo.
“Hiki
chama tukifika mahali tukaanza kufanyiana unafiki kwamba hatutaki
kuambiana ukweli tunapokosea utakuwa ndiyo mwanzo wa kuanguka kwa CCM.”
Amesema hayo juzi nyumbani kwake eneo la Kisasa mjini Dodoma katika mazungumzo maalumu na Mwananchi.
Nape
ambaye leo anatimiza miaka 40 ya kuzaliwa, ameeleza kusikitishwa na
namna ya baadhi ya watu aliowaita “vijana wa CCM”, kupotosha kwa
makusudi kauli na ujumbe wake anaoutuma kupitia mitandao ya Twitter na
Instagram.
“Kuna
ambao wanamchukia tu Nape kwa sababu wanadhani alishiriki kuzuia
wagombea wao na hasa hawa vijana wafuasi wa Edward Lowassa ambao bahati
mbaya alipohama hawakuhama naye,” alisema.
“Hawa
nao wako wanapitia humo kusema hasira zao. Mara Nape huyu anamsema
Rais. Unamuona Nape huyu anaisema Serikali. Hawa nao tuwapuuze. Wakikua
wataacha.
“Wanaona
Nape ni beki mzuri wa kufanyia mazoezi au ya kuonekana wapo ili tu
wapewe vyeo. Bahati nzuri mimi nimekulia ndani ya CCM najua lipi zuri na
lipi baya kwa CCM,” alisema.
Mbunge
huyo alisema husikitika anaposoma namna kauli zake zinavyopotoshwa,
huku wengine wakidai anatumia maneno makali kwa vile ameondolewa kwenye
uwaziri alikokuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Nape
alisema, “Hakuna jambo ambalo nimelisema kwenye Twitter na Instagram
ambalo halifai kusemwa. Wakati mwingine nina maneno magumu kwenye vikao.
Ninaamini kwenye hayo maneno magumu ndiko ambako tutakijenga chama
chetu,” alisema.
Alisema
akiwa katibu wa itikadi na uenezi kuna vikao vilifanyika mpaka saa sita
usiku na alikuwa mkorofi kidogo kwa sababu maneno yake wakati mwingine
yalikuwa magumu.
“Namshukuru
sana Kikwete (Rais mstaafu Jakaya) amenilea na amenivumilia wakati
mwingine, maana sarakasi nyingine na ujana huu amenivumilia sana,”
alisema.
Alisema,
“Katika watu wenye moyo wa ajabu sana ni Rais Kikwete (mstaafu). Katibu
mkuu wetu (Abdulrahman) Kinana naye ameni shape (nijenga) sana
kunivusha kutoka ujana hadi kukomaa.
“Lakini
nasema lazima CCM ijenge utamaduni wa kukosoana na kujikosoa ili tuende
mbele. Tukiua huo utamaduni tutakifanya hiki chama kitapoteza mwelekeo.
Tuujenge kwa nguvu kubwa.”
Akizungumzia
aina ya maneno anayoyatumia kufikisha ujumbe kupitia Tweeter, Nape
alisema ujumbe mzuri ni ule ambao ukiwekwa unafikirisha na unamfanya mtu
kueleza namna alivyouelewa.
“Tweet
nzuri ni ile ambayo ukiiweka inafikirisha. Tweet nzuri ya mtu
aliyetumia akili, ya mtu msomi huweki tweet ambayo kila mtu akisoma
umeandika shikamoo baba. Inatakiwa iwe ambayo mtu akisoma anafikiria na
anapata hamu ya kuitafakari. Nafurahi sana kwa sababu Tweet zangu
zinasumbua akili wakati mwingine wanapata majibu tofauti tofauti.
“Wengine
wananitukana wengine wananituhumu. Kwenye Tweet zangu hizi kwa sehemu
kubwa watu wanapotosha na wanaopotosha wamegawanyika katika makundi
mawili. Kuna ambao hawamjui Nape na hao ndiyo wale wanaosema Nape toka
(tangu) ametoka uwaziri ana tweet hivi lakini nimekuwa nikiwauliza kwani
kabla sijawa waziri, sijawa katibu mwenezi sikuwa nasema?”
“Wanasahau
mimi niliwahi kumnyoonyeshea kidole waziri mkuu wa Tanzania hadharani
nikasema wewe fisadi. Leo wanasema Nape anasema maneno makali sana! Hivi
kuna maneno makali zaidi ya kumnyooshea waziri mkuu wa nchi ukasema
hapa kwenye mradi huu umefanya ufisadi?
“Hawajui
mimi ndiye niliyesimama Songea nikasema Kikwete kuna mawaziri wako hapa
ni mizigo. Hivi kuna kauli kubwa ya kufikia hapo?
“Mtakumbuka
niliwahi kusimama kwenye mkutano wa hadhara lakini mtakumbuka
nilikwenda Arusha nikamwambia Lazaro (Nyalandu) nenda katimize wajibu
wako acha kuweka watetezi”.
Afikiria kujitoa mitandao ya kijamii
Akizungumzia
mkanganyiko wa namna watu wanavyopotosha ujumbe mbalimbali, Nape
alisema, “Pengine nitoke kwenye social media (mitandao ya kijamii)
sababu unaona kila mara uki-post (kutuma) jambo ooh linakuwa kubwa sana.
“Tena
wakati mwingine ni jambo la utani sana. Kwa mfano siku moja nimeangalia
kipindi kwenye televisheni wanasema mara paap na mimi nikaweka mara
paap.
“Nilipoweka
mara paap, wakaanza mara paap kahama CCM mara paap kafanya hivi, unakaa
unasema kwa nini wanafikiria negative (mabaya) kwa nini hawafikirii
positive (mazuri)?”
“Kwa
nini hawasemi mara paap ameimarisha chama... Ukiyaona haya naanza
kutafakari seriously (makini) umefika wakati nisimame kidogo hii social
media.”
Hata
hivyo alisema anaona akifanya hivyo atawapoteza wafuasi wake zaidi ya
200,000 walioko Tweeter na maelfu walioko Instagram na ndiyo maana
anajiuliza kwa nini atoke kwa sababu ya wapuuzi wachache?
Mbunge
huyo wa Mtama alisema pamoja na watu kutafsiri tofauti na kupotosha
maana halisi ya ujumbe wake, hajawahi kuitwa na chama chake kuhojiwa.
“CCM
ni chama kikubwa sana na mimi nimekaa humu zaidi ya miaka 10 nikiwa
mtumishi ukiacha miaka 20 nikiwa mwanachama. CCM ninaijua. Ninajua jambo
gani baya na jambo gani zuri.
Hata Nyerere aliiokosoa CCM
Alisema
si dhambi kuikosoa CCM ikiwa tu dhamira inakuwa ni kuijenga na
kuiimarisha na kwamba hata Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alikuwa
akiikosoa.
“Mwaka
1995 wakati mwalimu anazunguka kumnadi (Benjamin) Mkapa alikuwa anasema
CCM kokoro hili limebeba watu wote kuna wengine humu nikijiuliza
inakuwaje tuko chama kimoja nao. Yalikuwa maneno makali. Alienda Musoma
pale akasema nyie CCM mmesimamisha mgombea wenu pale mla rushwa. Huyu
mimi sitampigia kura nitampigia yule wa NCCR-Mageuzi.”
“Hivi
kuna maneno makali nimeyasema kuliko haya? Mwalimu alisema maneno
makali sana, lakini akasema kuna maneno ya uongo? Ni lazima tujenge
utamaduni wa kukosoana ili kujenga”
Mbunge
huyo alitumia mahojiano hayo kumpongeza Rais Magufuli kwa kutimiza
miaka miwili madarakani, lakini akasema upo mjadala wa namna
anavyotekeleza ilani ya CCM.
Nape
alisema yote yaliyoingizwa katika ilani ambayo Rais Magufuli
anaitekeleza kwa mafanikio, yalitokana na ziara yake yeye na Kinana
iliyowachukua miezi 36 ya kukiimarisha CCM.
“Tulipokuwa
tunazunguka yapo mambo mengi tuliyasema. Yale ndiyo yalikuja kuzaa
ilani ya uchaguzi ya CCM (2015-2020). Yale ndio yalikuja kuzaa mwelekeo
wa Serikali ya Awamu ya Tano.
“Sasa
hapa tunapotimiza miaka miwili, ukifanya tathmini mambo mengi
anayoyafanya Rais Magufuli pamoja na kumpongeza kwa kufikisha miaka
miwili, ni yale ambayo tuliyaweka kwenye ilani.”
Alisema
walipozunguka mikoani, wananchi walilalamikia kuhusu kuporomoka kwa
nidhamu ya utumishi wa umma, wingi wa sherehe za kitaifa, mikataba
mibovu ya madini na rushwa.
“Shida
ya nidhamu katika utumishi wa umma ilikuwa kubwa. Tuliikuta kila
mahali. Hili ni jambo moja Rais Magufuli amelisimamia vizuri,”alisema.
Aliyataja
maeneo mengine ambayo alisema Rais ameyasimamia vizuri kuwa ni
kudhibiti matumizi ya Serikali, kusimamia sera ya uchumi wa viwanda na
kushughulikia migogoro ya ardhi.
Maeneo
mengine ambayo alisema Rais amewafurahisha Watanzania ni kuondoa
utitiri wa kodi kwa wakulima, kudhibiti rasilimali ya madini na
kusimamia masilahi ya watumishi wa umma.
“Kwa
hiyo amefanikiwa kugusa kila mahali lakini mjadala uliopo ni namna
anavyoyatekeleza haya mambo. Hapa ndipo palipo na mjadala na watu wengi
wanazungumza hapo.
“Hili
mimi sitegemei watu wote watakubaliana. Wako wanaodhani angeenda
taratibu kidogo, wapo wanaodhani akaze zaidi, wapo wanaodhani afinye
zaidi na wako wanaodhani aende mdogomdogo.”
Nape
alisema hakuna ubishi nchi ilikuwa katika matatizo makubwa ya rushwa na
watu walitamani kupata kiongozi ambaye hataona aibu hata akimkuta
rafiki yake anafanya ufisadi amshughulikie.
“Tunadhani
Magufuli ameanza vizuri. Mjadala utakuja tu hivi katika utekelezaji
pengine tupunguze mwendo, twende kasi zaidi, tutumie busara zaidi,
tutumie upole fulani hivi. “Huu ndiyo mjadala ambao upo ambao nadhani si
mbaya lakini sio ambao unapaswa kumrudisha nyuma. Kwa tathmini yangu
mimi amefanikiwa kwa miaka hii miwili kutengeneza mwelekeo fulani.”
“Kitakachofuata
sasa hapa ni namna ya kuboresha utekelezaji wa yale tulioyaweka kwenye
ilani ya uchaguzi, yale ambayo ni matumaini ya Watanzania na yale ambayo
tuliwaahidi,” alisema.
Ajibu kauli ya Nyalandu CCM kupoteza mwelekeo
Akizungumzia
kauli ya Nyalandu kuwa CCM imepoteza mwelekeo, Nape alisema kwake
anadhani huo ni mtizamo wake na wala hataki kupuuza mtizamo wake huo
wala kuubeza.
“Na
mimi naamini CCM haijapoteza mwelekeo na mtakumbuka haya maneno
Nyalandu sio wa kwanza kuyasema. Aliwahi kuyasema Horace Kolimba miaka
hiyo na bado iko madarakani”
“Aliwai
kusema Kingunge Ngombale Mwiru kuwa CCM imeishiwa pumzi na bado
inapumua. Haya maneno ni mitizamo ya watu na Nyalandu anayo haki ya kuwa
na mtizamo wake,”alisema.
“Alipotoka
nilisema hivi kwamba aliibua hoja sita ukiacha hiyo ya kupoteza
mwelekeo. Nikasema hizi hoja zote alizoziibua zinazungumzika ndani ya
chama chetu. Angeweza tu kuzileta tukajadiliana”.
Kwa
sababu ukisema CCM imepoteza mwelekeo ukaandika paper (mada) ukaja nayo
ndani vikao uka justify (ukaitetea) ndio njia bora ya kurekebisha chama
na sio kuondoka,”alisema na kuongeza;-
“Ndio maana alipoondoka mimi nika tweet nikasema kama yapo mapungufu ndani ya CCM nitayashughulikia nikiwa ndani ya CCM”
“Mimi
katika utumishi wangu ndani ya CCM yako mengi sana ambayo nimeyasukuma
ndani ya chama na yametokea ikiwamo kuibadili kabisa ile idara ya
itikadi na uenezi”.
“Ninaamini
katika kuleta mabadiliko. Kila mmoja kwenye nafasi aliyopewa
akijitahidi kuleta mabadiliko fulani CCM itabadilika. CCM ya leo sio CCM
ya jana”.
“Ndio
maana kuna kauli mbiu CCM Mpya, Tanzania Mpya. Tunapotaka kuijenga
Tanzania mpya ni pamoja na fikra na mawazo. CCM mpaka leo haina mbadala
kwababu ya mfumo wake”.
Nape
alisema Chadema wamejitahidi kujenga msingi chini lakini wameshindwa na
chama chao kimebaki ngazi ya kitaifa zaidi lakini CCM ina uongozi hadi
chini ngazi ya balozi na shina.
“Lakini
CCM balozi wa nyumba kumi anajijua ni CCM na ndio nguvu ya CCM ilipo.
Hata uwezo wa kupanga. Ukitaka kuiua CCM lazima uue mfumo wake jambo
ambalo haliwezekaniki,”alisema.
“Kusema
CCM inapoteza mwelekeo ghafla sio sawa lakini kusema hakuna mapungufu
nayo sio sawa. Yapo mapungufu yanashughulikiwa na yanaweza kumalizwa na
vikao na mfumo wa chama”
“Haya
mapungufu ambayo pengine Lazaro aliyaona au wengine wanayaona dawa sio
kuyakimbia. Dawa ni kukaa kuyashughulikia. Wewe mwenzetu unayeona
yanakukera sana lete hoja”
Nape
alitolea mfano walipoingia kuwa Katibu Mwenezi, kulikuwa na kitengo cha
propaganda kilichokuwa kikiongozwa na watu waliotoka upinzani ambacho
alitoa hoja kikabadilishwa.
“Hiki
kitengo kilikuwa kinaongozwa na Tambwe Hiza. Moja ya jambo ambalo
lilikuwa linanikera sana ni kitengo hiki kuwa na historia ya kuongozwa
na watu waliotoka upinzani”
“Hili
lilikuwa moja ya jambo lilikuwa linapeleka sura mbaya kule nje.
Nilipoenda nikasema lazima tutoe hii. Tukaondoa propaganda tukatengeneza
mawasiliano na umma”
“Tukaweka
mawasiliano sio propaganda tu, kikaongozwa na Daniel Chongolo kwa muda
mrefu tu na akakijengea heshima kubwa sana na ndio hapo tukarudisha
mahusiano na vyombo vya habari”.
Nape
alisisitiza kuwa endapo kuna mwana CCM anayeamini katika itikadi yake
anayaona mapungufu fulani, ongeza nguvu ya kuleta hoja za mabadiliko
ndani ya chama na sio kukimbia.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment