NA TIGANYA VINCENT
RS-TABORA
4 December 2017
BODI ya Wakurugenzi
wa Bodi ya Tumbaku ya Tanzania imetakiwa kufuatilia malalamiko ya baadhi
ya wakulima ambao wamekuwa wakikataliwa kulima kwa sababu ya ueleza
ukweli kuhusu unyanyasaji unaonywa na Viongozi vyama vya msingi vya
wakulima wa tumbaku.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini
Tabora na Waziri wa Kilimo Dkt.Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa Bodi
ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku ya Tanzania.
Alisema kuwa
wakulima ambao wamekuwa wakifichua uovu unaofanywa na viongozi wa AMCOS
wamekuwa wakifanyiwa visasi ikiwa na kufutwa katika unachama na wakati
mwingine kuzuiwa kulima zao hilo.
Dkt. Tizeba
aliiagiza Bodi mpya kuhakikisha kuwa inawalinda wakulima wote wanafichua
madudu yanayofanywa na viongozi wachache kwa maslahi binafsi kwa ajili
ya ustawi wa zao hilo.
Alisema kuwa wasipolindwa wakulima ambao
wako mbele kusema ukweli uhai wa zao hilo unaweza kuwa mashakani kwa
kuwakumbatia viongozi wa vyama vya msingi ambao ni wabadhirifu
wanaogopwa.
Dkt.Tizeba alisema kuwa wakulima hao
wakikubaliwa kulima , tumbaku yao itapewa bei ya chini ili kuwaziba
midomo jambo ambalo ni uonevu.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine
wajumbe hao wanajukumu la kuhakikisha kuwa wakulima hawaonewi na
kunyanyasa na viongozi wao.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Kilimo
amewataka Bodi kuhakikisha kuwa wanasimamia wakulima wasije wakalima
tumbaku nje ya mkataba(makisio) ili kuepuka usumbufu wa kukosa masoko.
Alisema kuwa wakati Serikali ikiendelea
kutafuta masoko kwa wanunuzi wapya ni vema wakulima wakalima kulingana
na makubaliano ili matatizo yaliyojitokeza katika msimu uliopita na
kusababisha tumbaku kushindwa kununuliwa kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Hassan Wakasuvi alisema kuwa
watahakikisha hakuna mkulima atakayeonewa kwa kusema ukweli na kufichua
uovu.
Alisema kuwa bila uadilifu kwa viongozi wa vyama vya msingi na usimamiaji wa haki zao hilo litaendelea kuyumba.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment