NA TIGANYA VINCENT
RS-TABORA
4 DESEMBA 2017
WAKULIMA
wametakiwa kuhakikisha wanalima kilimo cha kisasa ambacho ndio
kitawawezesha kuzalisha ziada ambayo ndio itawaletea faida kwa ajili ya
kupata fedha za kujiletea maendeleo yatakayowaondoa katika umaskini.
Kauli
hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri
wakati wa uhamasishaji wa kilimo cha kisasa cha pamba na mazao mengine
katika maeneo mbalimbali.
Alisema
kuwa kilimo cha mazoea cha kuzalisha mavuno kwa ajili ya matumizi ya
kila siku tu hakiwezi kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao na
badala yake watakuwa wakitaabika pindi kunakuwepo na msimu mbaya wa
mavuno.
Mwanri
alisema kuwa ziada ndio itakayowasaidia kuleta maendeleo ikiwemo
kujenga nyumba nzuri za kisasa, kulala pa zuri kula vizuri na kuwa na
uwezo wa kuwaendeleza watoto wao kielimu.
Alisema
kuwa kilimo cha kimazoea hakiwezi kuwasaidia kupiga hatua bali
wataendelea kulima na kupata mazao ni kwa ajili ya kutumia wakati wa
mahitaji na sio kupata nyongeza kuuza kwa ajili ya kupata fedha za
shughuli nyingine za maendeleo.
Mwanri
alisema kuwa kwa kutambua kuwa kilimo kilichokuwa kinafanywa na
wakulima walio wengi cha kutozingatia utaalamu wa Maofisa Ugani
amewaagiza watumishi hao kwenda kwa wakulima vijijini ili waweze
kuwasaidia kubadilisha mtindo wao wa ulimaji na kuja na mbinu mpya za
kuwa na shamba dogo mavuno mengi.
“Mimi
siwezi nikakaa hapa ninajivunia kuwa Mkuu wa Mkoa wakati watu wangu
hawawezi kuzalisha ziada ambayo ndio itakayowawezesha kupata
maendeleo…ni lazima tutoke Maofisi twende tukafundishe wakulima juu ya
kilimo bora” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Alisema
kuwa ni vema Maofisa Ugani wakasaidia kuwafanya wakulima kuwa vifaa
(assets) na sio kuwa mizigo(liabilities) kwa kuwapa mbinu
zitakazowasaidia kupiga hatua kutoka walipo na kusonga mbele
kimaendeleo.
“Ningependa
kirudi hapa mwakani nikute habari njema za kuniambia kuwa kutokana na
elimu kutoka kwa Maafisa Ugani na viongozi mbalimbali mwaka huu nimepata
pamba nyingi hadi nimejenga nyuma hiyo hapo…hayo ndio maendeleo
tuyotaka…na sio kupata pesa unakwenda kulewa bila kufanya jambo lolote
la maendeleo” alisisitiza Mwanri.
Mkuu
huyo Mkoa wa Tabora ameamua kupitia katika vijiji mbalimbali
kuhamasisha juu ya kilimo cha kisasa cha mazao mengi kwa ajili ya kupata
malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vilivyopo na vinavyotarajiwa.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment