Home » » Mbunge Kiwanga aenda India kutibiwa moyo

Mbunge Kiwanga aenda India kutibiwa moyo


 
Mhe. Suzan Kiwanga (Chadema) 
MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga (Chadema) yuko nje ya nchi kwa matibabu ya moyo hali ambayo imesababisha kesi inayomkabili pamoja na washitakiwa wengine kuahirishwa hadi mwezi ujao. 


Taarifa hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki mahakamani ambapo Kiwanga pamoja na wanachama wengine watatu wa Chadema wanakabiliwa na mashitaka matatu ya jinai dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario. 

Washitakiwa wengine ni Sylivester Kasi; Mbunge wa Maswa Mashariki Sylivester Kasulumbayi, 
Anwar Kashanga na William Edward. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 30 mwaka huu.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo imeahirishwa kutokana na mshitakiwa wa pili, Kiwanga kuwa kwenye matibabu nje ya nchi. 

Kwa mujibu wa hakimu, amepokea taarifa ya maandishi kutoka kwa daktari inayoeleza kuwa Kiwango yuko India kwa matibabu ya moyo. 

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Mboneko Mugisha ulikubali ombi 
hilo na kuiambia Mahakama kuwa upo tayari kuendelea na kesi hiyo tarehe itakayopangwa. 

Mashitaka yanayowakabili ni matumizi ya lugha ya matusi, shambulio la madhara mwilini na kumweka chini ya ulinzi isivyo halali, tukio lililotokea Septemba mwaka jana wilayani 
Igunga wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga.


Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa