Home » » ASKARI JWTZ WANASWA NA MBAO ZA WIZI

ASKARI JWTZ WANASWA NA MBAO ZA WIZI

na Mwandishi wetu, Tabora
ASKARI wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Milambo mkoani Tabora, ni miongoni mwa watu tisa waliokamatwa na Kikosi cha Kuzuia Ujangili wakiwa na gari la serikali likiwa limesheheni mbao za magendo ndani ya hifadhi ya Ugala, Wilaya ya Urambo mkoani hapa.
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi ya Rasilimali za Misitu nchini (TFS), Vallentine Msusa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, askari hao (majina yamehifadhiwa kwa sasa) walikamatwa Ijumaa iliyopita saa mbili usiku wakiwa na gari lenye namba za usajili 5659 JW 09 aina ya IVECO wakiwa na mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa).
Msusa alisema kuwa kukamatwa kwa askari hao ni jambo la kusitikisha na ni aibu kwa taifa, na kuongeza kwamba gari lililokamatwa bado linahifadhiwa katika kambi iliyopo ndani ya pori la akiba la Kigosi likiwa na mbao 630 bila kibali.
Amebainisha kuwa siku za karibuni watu wengi wamekuwa wakitumia magari ya serikali kusafirishia maliasili za misitu kwa vile hayakaguliwi kwenye vizuizi na hivyo, kusababisha lawama kwa watumishi wa Wizara ya Maliasili kuwa ndiyo wahusika wa uvunaji holela.
“Tulitegemea taasisi za umma zingesaidia kutoa ulinzi wa misitu na rasilimali zilizomo kumbe sivyo,” alisema Msusa na kuongeza kuwa askari hao na watu wengine waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani ili wajibu tuhuma zinazowakabili.
Chanzo: Tanzania Daima   

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa