na Hastin Liumba, Sikonge
MKUU wa Wilaya (DC) ya Sikonge, mkoani Tabora, Hanifa Selengu, amemsweka ndani mtumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa madai ya kushindwa kuwajibika katika majukumu yake ikiwemo kutofuata maagizo yake.
Selengu alimuweka ndani Ofisa Utumishi Msaidizi wa halmashauri hiyo, Elly Arkechi kwa siku moja akimtuhumu kukwamisha kazi yake.
Tukio hilo lilitokea Agosti 29 mwaka huu, majira ya saa nane katika kikao cha kamati ya sherehe na maandalizi ya mbio za mwenge wa uhuru.
Akizungumza na Tanzania Daima, Arkechi, alisema ni kweli alilala ndani saa 24.
“Tulikuwa kwenye kikao cha kamati ya sherehe, tukijadili maandalizi ya mbio za mwenge wa uhuru… sasa mimi na mwenzangu afisa utamaduni, Exavery Malapwa tuko kwenye kamati ya usafirishaji ndipo sheshe lilipoanzia,” alisema.
Arkechi alisema walipishana kauli wakati anamuelekeza kuhusu kamati ya usafirishaji, lakini DC huyo alikuja juu na kusema maagizo yake yamepuuzwa.
Alisema wakiwa kwenye mjadala, ghafla DC huyo alimwagiza mwakilishi wa OCD Bayo amkamate akamweke ndani.
Akizungumzia tukio hilo, Arkechi alisema amepeleka malalamiko yake Baraza la Wafanyakazi ili lifanyiwe kazi kwani anaona amedhalilishwa.
Alipotafutwa DC huyo kuzunguzia suala hilo, alisema kwa kifupi: “Nimekusikia, sina cha kusema nipo safarini naenda kwenye msiba.”
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment