Home » » RAGE AWATOLEA UVIVU WANASIASA

RAGE AWATOLEA UVIVU WANASIASA

Rose Mweko, Tabora
MBUNGE wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage amewataka wanasiasa wanaobeza kuwa, Rais Jakaya Kikwete hajafanya kazi yoyote ya maendeleo, kuacha maneno hayo mara moja.

Rage ameyasema hayo, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalunde, wakati akigakua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati na ghala la kuhifadhia tumbaku.

Alisema Rais Kikwete, amefanya mambo mengi makubwa yanayopaswa kupongezwa na wananchi.

“Nawashangaa wanasiasa uchwara wanaodai eti Rais Kikwete hajafanya kituo chochote katika nchi hii… bila kupanga hoja za msingi hivi na sisi tukiamua kuanza kutoa lugha za aina hii kweli taifa hili litakuwa taifa kama lilivyo,… mpaka sasa watu hawaoni miradi ya barabara inayoendelea nchi nzima, ina maana hawaoni zahanati na shule zinazofunguliwa tena zenye vifaa vya kisasa jamani, siku zote haki huendana na wajibu, hivyo nawaomba waache kutukana, kwani huu si utamaduni wa Mtanzania,” alisema Rage.

“Rais ni kielelezo cha taifa, wanasiasa hawa wasichukulie upole na hekima ya Rais kukaa kimya, wakaona ni njia ya kujipatia umaarufu kwa kukosa adabu, tunapaswa kushindana kwa hoja na sio matusi,” alisema Rage.

Alisema anaungana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) aliyesema wabunge vijana wote ambao hawakupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), umefika wakati wa kwenda sasa.

Alisema Zitto ni mwanasiasa aliyekomaa kutokana na jinsi anavyopanga hoja zake bila kumkosea mtu adabu wala kutoa lugha ya kuudhi.

Katika hatua nyingine, Rage alimtaka mkandarasi anayejenga zahanati ya Kalunde, kuhakikisha anakabidhi jengo hilo, ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa, lasivyo atachukuliwa hatua za kisheria kutokana na kuchelewesha ujenzi.

Naye, Diwani wa Kata ya Kalunde, Jumanne Simende alisema tangu Aprili mwaka huu, hawajawahi kumuona mkandarasi huyo, licha ya kulipwa fedha zote.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa