Mwandishi
wetu, Sikonge-Tabora Yetu
Utumikishwaji
watoto katika mashamba ya tumbaku na ufugaji wa ng’ombe katika jamii za
Wasukuma na Wanyamwezi wilayani Sikonge Mkoani Tabora imepungua kutoka asilimia
90 hadi kufikia asilimia 50, baada ya elimu kutolewa kwa jamii.
Hayo yamesemwa
na Bw. Ezekiel Basisi, mhamasishaji na mshauri wa Prosper kata ya Ipole, kwenye
sherehe ya uelimishaji jamii kuondoa watoto katika utumikishwaji wa kilimo cha
tumbaku iliyofanyika katika kijiji cha Udongo, kata ya Ipole wilayani Sikonge
na kuhudhuriwa na wakazi wa vijiji vya Makazi na Mitwigu.
Aidha Bw,
Basisi amesema licha ya kutoa elimu juu ya kuacha kutumikisha watoto katika
jamii ya wafugaji, mashambani, majumbani na kazi zinginezo, pia mradi wa
Prosper umekuwa ukishirikiana na halmashauri ya wilaya Sikonge kutoa
elimu ya mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 17
na vikundi mbalimbali vya akina mama.
Meneja wa
Prosper, Bw, Christoher Luyenga, amebainisha kuwa mradi huo
umefanikiwa kutoa mikopo kwa vikundi 10 vya wakinamama wajasiriamali toka
vijiji mbalimbali wenye thamani ya sh. mil 43.5 kwa ajili ya kuendesha
biashara ndogo ndogo ili kuwakwamua kutoka katika umaskini wa kipato.
Bw, Luyenga
amesema kuwa mbali na kusaidia wajasiriamali, mradi huu pia umefadhili watoto
wa shule za msingi wapatao 300 katika vijiji hivyo, ambapo vifaa mbalimbali vya
shule na gharama nyinginezo zenye thamani ya sh milioni 15 vimetolewa kwa
watoto hao na vinaendelea kutolewa mpaka watakapomaliza shule, lengo la madi
huu ni kufadhili watoto wapatao 600.
Kwa upande
wake Mratibu wa Prosper Wilayani Sikonge, Bi. Jesca Kibiki amesema lengo ni
kuihamasisha jamii na kuijengea uwezo ili ipambane na ajira mbaya kwa watoto,
ikiwa ni pamoja na kuihamasisha kulima zao hilo la tumbaku bila kutumikisha
watoto.
Amesema mradi
huo wa kupambana na utumikishwaji watoto hapa mkoani Tabora, ni mradi wa
miaka 4 na umefadhiriwa na taasisi ya kimataifa ya ECTL yenye makao makuu
jijini Geneva, nchini Uswisi na umeanza mwezi Des.2011 na unatarajiwa kufungwa
Des.2015.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment