Zitto Kabwe
WAKATI
ripoti ya kamati iliyoundwa na serikali kuchunguza tuhuma za vigogo
walioficha fedha kwenye mabenki ya nje ya nchi ikiwa bado haijatolewa
bungeni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amewataja
vigogo watatu kuwa miongoni mwa wahusika.
Zitto
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), ndiye muasisi wa hoja
hiyo bungeni. Hivi karibuni alitishia kuwataja wahusika endapo serikali
haitawasilisha ripoti hiyo kwenye mkutano wa Bunge uliomalizika
Jumamosi.
Mbunge
huyo aliwataja vigogo hao juzi wilayani Kaliua mkoani Tabora wakati
akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Uwanja wa Kolimba.
Bila
kutaja majina yao, Zitto aliwataja kwa nyadhifa zao walizowahi kushika
akisema ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ulinzi
wa zamani na aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi.
Alisema
baada ya kutoa hoja bungeni ya kuitaka serikali ifanye uchunguzi juu ya
Watanzania walioficha fedha nje ya nchi, alichaguliwa kuongoza timu ya
kufuatilia sakata hilo, kupitia taasisi ya Eurodad, ambapo alifanya
ziara katika sehemu mbalimbali ikiwemo nchini Uswisi na Uingereza.
Zitto
alifafanua kuwa akiwa huko alikutana na wadau mbalimbali wa masuala ya
kibenki pamoja na kuhudhuria mkutano wa Waziri Mkuu wa Uingereza
uliokuwa ukizungumzia utoroshwaji wa fedha.
“Hawa
watu wanajulikana na tutawataja kwa majina mchakato ukikamilika, lakini
kwa sasa niwaambie miongoni mwa watu hao ni pamoja na waliowahi kuwa
mawaziri na mmoja wa wakuu wa majeshi mstaafu,” alisema Zitto.
Alisema
kutokana na hali hiyo, serikali inaendelea kushikwa na kigugumizi cha
kuwaanika watu hao hadharani licha ya Serikali ya Uswisi kuitaka isaini
mkataba wa kubadilishana taarifa.
Zitto
alisema kwa sasa ameshawaagiza wasaidizi wake katika masuala ya kibunge
kuandika utaratibu utakaowasilishwa bungeni kwa ajili ya kuwadhibiti
watu wanaoficha fedha nje bila kuwa na maelezo ya kutosha.
Aliongeza
kuwa suala la kuwaanika hadharani watu wanaoficha fedha nje ya nchi
linahitaji uungwaji mkono wa hali ya juu kwa kuwa ni kazi ya hatari
inayowagusa watu wenye maslahi na uwezo mkubwa nchini.
Kwa
mujibu wa mbunge huyo, mbali na Tanzania, nchi nyingi za Afrika zinaweka
fedha nyingi Uingereza pamoja na visiwa vyake 15 ambapo katika kisiwa
cha Jersey pekee kuna paundi bilioni 40 za Uingereza.
Zitto
alisema baadhi ya nchi huwafilisi watu ambao wanabainika kuwa wameficha
fedha nje na kuzitumia kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema
kuwa wakati anafanya shughuli hiyo aliyosema ni ajenda ya kitaifa,
alitegemea kuungwa mkono na watu wake wa karibu, ikiwa ni pamoja na
walio ndani ya chama chake.
“Hivi ni
vita visivyohitaji utengano, tunapoamua kulumbana sisi kwa sisi wenzetu
wanapata mwanya wa kufanya mambo yao, nilitegemea katika hali hii
CHADEMA tushikamane kuliangamiza hili dude CCM,” alisema Zitto.
Kuhusu migogoro
Zitto
alisema CHADEMA hawama migogoro na kinachofanyika ni mikakati ya watu
wachachahe wasio na shughuli kuamua kuwagonganisha viongozi.
“Kuna
watu wachache sana ambao hawana kazi, shughuli yao ni kugonganisha
viongozi ili wagombane na ikitokea hivyo wao ndiyo furaha kwao, sio
ufahari hata kidogo kwa CHADEMA kuonekana ina migogoro,” alisema.
Zitto
alisema mwaka 1995 kabla ya CHADEMA kuamua kuiunga mkono NCCR-Mageuzi,
Edwin Mtei na Bob Makani waligombea nafasi ya kutaka kuwania urais
kupitia chama hicho na hakukuwa na misigano yoyote kwa kuwa walijua
malengo yao ni kuwatumikia Watanzania.
Aliongeza
kuwa hali ya watu kuwania nafasi moja ndani ya CHADEMA ilijirudia mwaka
1998, kwa nafasi ya uenyekiti kuwaniwa na watu wawili tofauti na
hakukuwa na mgogoro.
“Uchaguzi
ndani ya CHADEMA ulifanyika mwaka 2009, tukapata viongozi na tukaingia
kazini, mliona tulichofanya, tulivuna wabunge wengi, madiwani na
wenyeviti wa mitaa. Lakini sasa hali inaanza kuwa ya ajabu ajabu
utafikiri kuna mtu aliyetangaza kugombea,” alisema.
Kwa
mujibu wa Zitto, hatua yake ya kugombea uenyekiti mwaka 2009 ilitokana
na kile alichokuwa amekiona kuwa kutekeleza demokrasia ndani ya chama
chake kutokana na waliomtangulia kujitokeza kuwania nafasi walizoona
zinawafaa.
“Mimi ni
binadamu, nina damu na nyama, katika umri huu mdogo nimepigwa mishale
mingi sana ya kisiasa, ninaumia na damu inanitoka, sasa nimechoka
kupigwa mishale, ni lazima viongozi tuambiane ukweli na tukemee hali
hii,” alisema Zitto.
Alisema
kuwa mwanzoni hapakuwa na chama chenye nguvu kama NCCR-Mageuzi, lakini
walipoanza kupigana kile alichokiita mishale, chama hicho
kilisambaratika.
“Wakamchafua
sana Mabere Marando kuwa ndiye msaliti, sasa Marando yuko wapi? Si ni
kamanda wetu? Si ndiye huyu mwanasheria wetu? Lazima tuambiane ukweli na
tuweze kuvikwepa vihunzi vya CCM, lazima sasa wanachama wanaoleta
chokochoko washughulikiwe,” alisema.
Alisema kuwa viongozi lazima waonye haya mambo, kwamba bila kuonya wataonekana wanashiriki.
“Waha tuna msemo; ukiona kifaranga yupo juu ya chungu, jua mama yake yupo chini,” alisema Zitto.
Kapuya ajisalimisha
Katika
hatua nyingine, Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM),
juzi alijisalimisha katika ofisi ya CHADEMA akimuomba Zitto azungumzie
matatizo ya barabara katika jimbo lake ili aweze kusaidiwa.
Kapuya
alitoa ombi hilo katika ofisi za CHADEMA wilaya baada ya Zitto kuwasili
eneo hilo saa 9.30 mchana kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara, ikiwa
ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati alipohutubia mkutano wa awali
kwa njia ya simu wiki tatu zilizopita.
Akiwa
ofisini hapo, Prof. Kapuya alihojiwa na Zitto akitaka kujua sababu ya
kuikodishia Halmashauri ya Kaliua nyumba yake huku akiwa ni mmoja wa
madiwani wa wilaya hiyo wanaopaswa kuhakikisha halmashauri inakuwa na
majengo yake.
“Karibu
mzee katika ofisi zetu, lakini unaweza kuniambia kama uamuzi wako wa
kuikodishia halmashauri nyumba yako hauingiliani na vikwazo vya
kuiwezesha kupata majengo yake?” alihoji Zitto.
Katika
kujitetea, Prof. Kapuya alisema sababu ya kufanya biashara hiyo na
halmashauri ni kutokana na wilaya kutokuwa na majengo yake binafsi.
“Ni kweli
mimi ninakodisha, lakini kiasi ninachochukua ni kidogo kuliko kile
anachochukua Waziri Magufuli katika Wilaya ya Chato, kwani naye
anaikodishia halmashauri ya wilaya yake jengo linalotumika kama ofisi,”
alisema Kapuya.
Katika
hali ya kuonyesha kuwa anaomba Zitto asizungumzie upungufu uliopo katika
jimbo lake, Prof. Kapuya alimuomba azungumzie matatizo ya barabara.
Zitto
alisema kimaadili kiongozi anapofanya biashara sehemu anayoweza kuwa na
uamuzi inasababisha hali ya kulinda maslahi ya kiongozi huyo ikiwa ni
pamoja na kukwamisha mradi wa eneo husika usikamilike au kujiongezea
gharama katika biashara husika.
Alimueleza
Prof. Kapuya kuwa kinachosabaisha Mkoa wa Tabora usiendelee, ni pamoja
na matatizo ya ubinafsi kati ya wabunge wa mkoa huo, huku akiwaambia
waache tofauti zao na Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta katika
kuwatumikia wananchi.
CHANZO: JUMA MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment