Tabora. Bodi mpya ya Chama Kikuu cha Ushirika
wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (Wetcu Ltd), imependekezwa
kuvunjwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwamo
kushindwa kulipa madeni ya wakulima.
Azimio la kuvunjwa kwa chama hicho kinaongozwa na
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi,
limetolewa na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Katika kikao hicho wajumbe walionyeshwa
kusikitishwa jinsi bodi hiyo yenye jukumu la kusimamia masilahi ya
wakulima wa tumbaku, inavyoendelea kuwakandamiza.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisema Wetcu Ltd
inapaswa kulaumiwa kwa sababu imepewa jukumu la kuhakikisha matatizo
yote yanayowakabili wakulima wa tumbaku na vyama vyao vya msingi
yanatatuliwa, lakini hali imekuwa kinyume.
“Wetcu imeshindwa kabisa kuwasaidia wakulima,
madeni yao ni makubwa hayajalipwa mpaka sasa kwa wilaya zote za Tabora.
Hali hii inazidi kuwaongezea umaskini mkubwa tunatakiwa kuchukua hatua,”
alisema Mkumba.
Alisema Wetcu imeshindwa kuweka mikakati endelevu
na haina nia ya dhati kuondoa kero zinazomkabili mkulima, badala yake
inamuongezea mzigo wa madeni.
Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM)
alipongeza hatua ya Mkuu wa Mkoa huo, Fatma Mwassa kuleta timu ya
wakaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG)
kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya Wetcu.
“Mwenyekiti nakupongeza kwa kutuletea timu ya
wakaguzi kutoka Ofisi ya CAG, naomba uchunguzi huo ufanyike haraka na
watakaobainika kuhusika na wizi wa fedha za wakulima kupitia chama hicho
wachukuliwe hatua kali,” alisema Tambwe.
Akizungumzia taarifa za uchunguzi wa zao hilo, Dk
Phillips Mtiba ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi), alisema
kitendo cha wakulima wengi kutolipwa fedha zao kinawasababishia umaskini
ambao hawakutarajia.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Fatma Mwassa alisema bodi
ya Wetcu iliwekwa na Wizara ya Ushirika na Masoko kwa muda, hivyo ipo
haja ya kufanya uchaguzi mpya kwa sbabu imeshindwa kutekeleza majukumu
yake ipasavyo.
Aliongeza kuwa bodi hiyo imekuwa ikitoa zabuni kwa
upendeleo, imeshindwa kulipa madeni ya wakulima hali ambayo
inawaongezea ugumu wa maisha wakulima hao kwa kuwalimbikizia madeni, na
kwamba kwa ujumla haiwatendei haki.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment