Na Hastin Liumba, Sikonge
WILAYA ya Sikonge mkoani Tabora imedhamiria kumaliza kero katika
utoaji huduma za wananchi kwa kuweka vipaumbele katika sekta za elimu,
afya na miundo mbinu ya barabara.
Hayo yalibainishwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya (DCC),
kilichoketi wilayani humo.
Akitoa taarifa katika kikao hicho Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
ya wilaya hiyo Shadrack Mhagama aliwaambia wajumbe hao kuwa
halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa katika sekta ya
elimu, afya na nyinginezo lakini akasema wamejipanga vizuri
kukabiliana nazo.
‘Ndugu zangu napenda kuwajulisheni kwamba tumedhamiria kushughulikia
mapungufu yote yaliyopo katika huduma za afya, elimu, barabara na kwa
lengo la kuwaondolea kero hizo,tumeandaa bajeti inayozingatia haja na
kukidhi vipaumbele vya kumaliza kero hizo’,
alisema.
Alisema katika bajeti hiyo wametenga kiasi cha sh 8,712,563,018 ili
kuboresha elimu ya msingi na sekondari katika shule mbalimbali
wilayani humo hususani uimarishaji wa miundo mbinu ya shule hizo
kupitia ujenzi wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, maabara na
vifaa vyake vyote pamoja na mishahara ya walimu.
Katika kuboresha sekta ya afya, alisema jumla ya sh 2,280,674,184
zimetengwa kukamilisha ujenzi wa vituo mbalimbali vya afya na
kuboresha miundo mbinu ya kituo cha afya Mazinge, ununuzi wa x-ray,
kujenga maabara, wodi ya watoto,kina mama na ujenzi wa njia za kupitia
(corridor), mradi wa kuvuna maji na mishahara.
Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha huduma za maji safi na
salama ambapo miradi mbalimbali ya maji itakarabatiwa ikiwemo mradi wa
Usunga sambamba na uendelezaji ujenzi wa miradi mingine ikiwemo mradi
wa Kitunda na Ulyanyama ambapo jumla ya sh 90,000,000 zimeombwa.
Vipaumbele vingine ni kuendeleza mradi wa kituo cha vijana (Pathfinder
Green City) kwa kujenga majengo, miradi ya mashamba na mradi wa maji
ambao umeombewa kiasi cha sh bil 1.
Aliongeza kuwa halmashauri hiyo pia imedhamiria kuboresha mbinu za
ukusanyaji wa mapato ya ndani na kujenga soko la wilaya ili kuongeza
mapato ya halmashauri sambamba na kujenga vituo vya polisi na mahakama
ili kuimarisha ulinzi na usalama wilayani humo.
Ili kuimarisha miundo mbinu ya barabara alisema wameainisha njia zote
korofi na madaraja katika maeneo hayo na kuahidi kuwa watafanya kila
linalowezekana ili ukarabati ufanyike katika barabara na madaraja
hayo, japo alikiri mbele ya wajumbe kuwa kikwazo kikubwa ni ufinyu
wabajeti.
Aidha alibainisha kuwa halmashauri hiyo pia inaandaa mpango kabambe wa
ukuaji wa Mji wa Sikonge (Master plan) utakaohusisha upimaji wa
viwanja na ulipaji fidia kwa wananchi wa Mji wa Sikonge.
Home »
» SIKONGE YAWEKA VIPAUMBELE UTOAJI HUDUMA.
0 comments:
Post a Comment