Home » » WILAYA YA SIKONGE YADHAMIRIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NA ELIMU‏

WILAYA YA SIKONGE YADHAMIRIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NA ELIMU‏

Na Allan Ntana, Sikonge
 
HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora imedhamiria kumaliza
kero zote zinazowakwaza wananchi katika maeneo mbalimbali ya utoaji
huduma hususani katika sekta ya elimu, afya, miundo mbinu ya barabara
na nyinginezo.
 
Hayo yalibainishwa katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya, DCC,
kilichoketi jana mjini hapa na kuhudhuriwa na Kaimu DAS, Mwenyekiti wa
halmashauri, Mbunge wa Sikonge, Mkurugenzi, Madiwani, Watendaji wakuu
wa idara, wawakilishi wa vyama vya siasa, taasisi za kidini, NGO’s,
mashirika na wananchi wa kawaida.
 
Akitoa taarifa katika kikao hicho Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
ya wilaya hiyo Shadrack Mhagama aliwaambia wajumbe hao kuwa
halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa katika sekta ya
elimu, afya na nyinginezo lakini akasema wamejipanga vizuri
kukabiliana nazo.
 
‘Ndugu zangu napenda kuwajulisheni kwamba tumedhamiria kushughulikia
mapungufu yote yaliyopo katika huduma za afya, elimu, barabara na
nyinginezo kwa lengo la kuwaondolea kero hizo,tumeandaa bajeti
inayozingatia haja na kukidhi vipaumbele vya kumaliza kero hizo’,
alisema.
 
Alisema katika bajeti hiyo wametenga kiasi cha sh 8,712,563,018 ili
kuboresha elimu ya msingi na sekondari katika shule mbalimbali
wilayani humo hususani uimarishaji wa miundo mbinu ya shule hizo
kupitia ujenzi wa nyumba za waalimu, madarasa, maabara na vifaa vyake
vyote pamoja na mishahara ya waalimu.
 
Katika kuboresha sekta ya afya, alisema jumla ya sh 2,280,674,184
zimetengwa   kukamilisha ujenzi wa vituo mbalimbali vya afya na
kuboresha miundo mbinu ya kituo cha afya Mazinge, ununuzi wa x-ray,
kujenga maabara, wodi ya watoto, ya akina mama na akina baba, ujenzi
wa njia za kupitia (corridor), mradi wa kuvuna maji na mishahara.
 
Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha huduma za maji safi na
salama ambapo miradi mbalimbali ya maji itakarabatiwa ikiwemo mradi wa
Usunga sambamba na uendelezaji ujenzi wa miradi mingine ikiwemo mradi
wa Kitunda na Ulyanyama ambapo jumla ya sh 90,000,000 zimeombwa.
 
Vipaumbele vingine ni kuendeleza mradi wa kituo cha vijana (Pathfinder
Green City) kwa kujenga majengo, miradi ya mashamba na mradi wa maji
ambao umeombewa kiasi cha sh bil.1.
 
Aliongeza kuwa halmashauri hiyo pia imedhamiria kuboresha mbinu za
ukusanyaji wa mapato ya ndani na kujenga soko la wilaya ili kuongeza
mapato ya halmashauri sambamba na kujenga vituo vya polisi na mahakama
ili kuimarisha ulinzi na usalama wilayani humo.
 
Ili kuimarisha miundo mbinu ya barabara alisema wameainisha njia zote
korofi na madaraja katika maeneo hayo na kuahidi kuwa watafanya kila
linalowezekana ili ukarabati ufanyike katika barabara na madaraja
hayo, japo alikiri mbele ya wajumbe kuwa kikwazo kikubwa ni ufinyu wa
bajeti.
 
Aidha alibainisha kuwa halmashauri hiyo pia inaandaa mpango kabambe wa
ukuaji wa Mji wa Sikonge (Master plan) utakaohusisha upimaji wa
viwanja na ulipaji fidia kwa wananchi wa Mji wa Sikonge.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa