Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ikifikia wakati kila uamkapo asubuhi unajikuta na maswali mengi
ya kujiuliza kuhusu maisha kuliko majibu, hapana shaka kitakachofuata ni
kuchanganyikiwa.
Ndivyo medani yetu ya michezo ilivyo. Kila siku
tunaamka na maswali mapya ya kujiuliza kuhusu hatima yetu. Tunalimbikiza
maswali yasiyo na majibu. Siyo timu za taifa, klabu wala viongozi.
Maswali ni kila siku.
Na ukitaka kujaza maswali kichwani mwako, jaribu
kuwauliza viongozi wetu, au kosoa utendaji wao. Utaonekana mbaya,
mchokonozi usiyestahili kuvumiliwa katika jamii. Ndiyo maisha ya medani
ya michezo nchini.
Viongozi wamejisahau. Hawatimizi wajibu wao na
hawataki kuulizwa kuhusu lolote kwenye uongozi wa umma. Wanataka kila
kukichwa washuhudie wameandikwa vizuri.
Wanataka hata kwenye ubaya wa utendaji wao,
waandikwe vizuri, wapambwe waonekana ndiyo viongozi bora. Sasa kwa hali
hii, utakosaje maswali mengi ya kujiuliza kuliko majibu?.
Utamaduni wao mbaya wa kung’ang’ania madaraka na
kujenga misingi ya kubebana katika kuongoza taasisi na klabu mbalimbali
za michezo ni hatari kwa maendeleo ya ustawi wa michezo nchini.
Leo hii kuna viongozi wameganda kwenye uongozi
miaka nenda, rudi. Hakuna walilofanya kuletea mafanikio. Shutuma za
uongozi mbaya dhidi yao haziishi kusemwa. Zinasemwa asubuhi, mchana na
hata usiku.
Na ukitaka kuchafua hali ya hewa, waambie
wajiuzulu kwa vile wameshindwa kusimama kwenye mstari wa dhamira ya
mafanikio. Watakuwa wakali na kukuhoji kwa nini unawafuatilia sana.
Watakuacha na maswali mengi ya kujiuliza kuliko majibu. Ndipo tulipofika
sasa katika medani ya michezo. Inashangaza kuona baadhi ya viongozi
wakijisahau, hawakumbuki walikotoka. Wameufanya uongozi wa umma kuwa
binafsi. Hawataki kukosolewa, wagumu kukubali makosa. Mpaka lini maswali
haya?.
Hata kama inatokea wameboronga katika utendaji wao
na kutakiwa kuwajibika, hakuna anayeweza kufaya hivyo. Kwa nini
wajiuzulu? Halafu aongoze nani wakati vyeo vimeandikwa majina yao?.
Nikumbushe. Kiongozi bora ni yule anayefuata
misingi bora ya uongozi, atakayekuwa na tafsiri sahihi ya uongozi ni
dhamana. Atayeiheshimu katiba na kuifanya kuwa kielelezo bora cha
uwajibikaji.
Atakayekuwa tayari kuwajibika ashindwapo kutimiza
malengo ya uongozi, atakayeongoza kwa tija ya umma na siyo kinyume
chake. Angalau haya yakifanyika tunaweza kupunguza wingi wa maswali.
Majibu hayatatusumbua. Na hatari ya kuchanganyikiwa tutajitenga nayo.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment