Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waislamu nchini na duniani kote, leo wanaungana kusherehekea
sikukuu ya kuadhimisha ibada tukufu na kongwe ya mwezi baada ya
kumalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kila Mwislamu anapaswa kumshukuru mola wake kwa
kusema “Alhamdulillah” kumwezesha kuifunga ramadhani kwani wapo wengi
ambao wangependa kutekeleza ibada hii, lakini hawakuweza kwa matatizo
mbalimbali, magonjwa, vita, vifo, ajali na majanga ya njaa na ukame.
Ni kweli kabisa kila aina ya sifa na shukrani
zinastahili kwenda kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba kutokana na
ukarimu na mapenzi yake kwa kuwawezesha watu wake kuukamilisha mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kufikia siku adhimu ya kufurahi,
kupongezana, kusaidiana, kushirikiana na kuoneana huruma. Ni siku ya Idd
El Fitri, Allah azikubali funga za wafungaji wote.
Huu ni wakati wa waumini wa dini ya Kiislamu
nchini kuungana na wenzao duniani kote kusherehekea sikukuu hii ya Idd
El Fitri baada ya kukamilisha ibada kongwe ambayo pia iliwajibishwa na
kutekelezwa na watu (umma) waliowahi kuishi katika hii dunia kabla ya
Muhammad (S.A.W). Hivyo ipo kila sababu na haja ya kumuomba Mwenyezi
Mungu azipe nguvu na imani nafsi za wafungaji ili ziepukane na fitna,
maovu, husda, ukatili na mabalaa mbalimbali ya nyuma na mbele yao,
angani na ardhini, kulia na kushoto.
Aidha, siku hii ni ya kumwomba Mwenyezi Mungu
awajalie mioyo ya huruma wafungaji wote waliojali ndugu, jamaa,
marafiki, watu wenye mahitaji maalumu kama vile wenye ulemavu, mafukara
na maskini kwa kuwapa misaada mbalimbali, zaka na hata sadaka ili
wasijione madhalili, wanyonge, wapweke na wenye huzuni katika siku hii
ya furaha.
Siku ya Idd ni siku ya kuwaangalia kwa jicho la
huruma wagonjwa waliomo majumbani na hata hospitalini, wafungwa
magerezani kwa kuwatembelea na kuwasaidia kwa kila hali sambamba na
kuwaombea dua ya kuwatakia afya njema, nusura ili wamshukuru Mwenyezi
Mungu na wajione ni sehemu muhimu katika sherehe hii.
Ni siku ya Waislamu kupongezana kwa kumaliza
mfungo wa Ramadhani kwa kuwa ndio lengo la kuifuatishia kwa zaka ya
chakula muhimu kinachopendwa katika mji au jamii husika ambacho kwa
Tanzania chakula hicho ni mchele.
Ndani ya Ramadhani Waislamu walichukua ahadi kwa
ajili kutekeleza ibada ya Funga kwa kujinyima mambo mbalimbali
waliyohalalishiwa, ikiwa ni pamoja na kula, kunywa au makutano ya
wanandoa mchana wa Ramadhani. Basi leo, Waislam wameruhusiwa kujinafasi
kwa mambo hayo na ipo faida kubwa kwa aliyefunga.
Imezoeleka kuzungumzwa katika jamii kwamba, uhuru
bila ya mipaka husababisha maafa. Hivyo ndio maana Mwenyezi Mungu
ameweka mipaka katika kusherehekea Sikukuu ya Idd. Hivyo wale ambao
watajipa mamlaka na uhuru kupita kiasi na kusahau mipaka ya Mwenyezi
Mungu mwenyewe anawaona na anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao.
Miongoni mwa matukio muhimu ya Sikuu hii ya Idd ni
kwa Muislamu kushiriki katika swala maalumu ya Idd ambayo hufuatiwa na
hotuba kama njia ya kufanya tathmini na kukumbushana, kuhamasishana,
kuelekezana na kusisitizana katika kuendeleza utiifu, wema, ukarimu,
upendo na heshima iliyojengwa ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama
chuo.
Ama wale ambao watafanya fujo katika siku hii
wakidhania kwamba ndio wamefika na wakaamua kuzikomoa swaumu zao kwa
matendo maovu, hao watakuwa na tathmini mbovu na watakuwa wameshinda
njaa tu lakini hawakufunga, kwani funga humwandaa mtu kuwa mcha Mungu.
Hivyo, wale wote ambao lengo hilo halikufikiwa
wanapaswa kujuta, kulia na kumwomba msamaha Mwenyezi Mungu. Ewe Muislamu
unayo kila sababu ya kujiepusha na kumuasi Mwenyezi Mungu baada ya
mfungo kwani mwenye kufanya hivyo ni sawa na aliyemuasi Mwenyezi Mungu
siku ya malipo
Walioelewa maana ya swaumu na kulifikia lengo lake ndio wale
wanaoendeleza mafunzo yake. Wapo wengi waliotumia fedha nyingi kwa
kupamba na kukarabati misikiti, kufuturisha watu, kukirimu na
kuwahurumia wenzao, kutoa zaka na sadaka kwa wahitaji wakatiu wa mwezi
mtukufu.
Ni siku ya furaha, lakini ipo haja ya kuwakumbuka
baadhi ya waumini ambao licha ya kula na kunywa, bado hawana furaha
ndani ya nafsi zao kwa kuwa na dhiki mbalimbali za kilimwengu kama
wafungwa magerezani, waliopata maafa ya ajali za ardhini na angani,
wagonjwa hospitalini na walio katika vita kama walivyo Wapalestina hivi
sasa.
Wote hawa wangetamani kuungana na wenzao katika
siku hii ya furaha, lakini hawakuweza, Allah awape subra, nusura,
msamaha na imani kubwa kwake ila wafanikiwe.
Ni siku ya kuiendeleza ahadi uliyoichukua ndani ya
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kama uliipenda swala, kusoma Quran,
kusimama usiku, kukaa itikafu, kukirimu watu, kusaidia wanyonge,
kuhurumia wasiojiweza na ukachukia zinaa, dhuluma, rushwa, kusengenya,
kusema uongo, kunywa pombe na kuiba.
Ewe Muislamu usijiweke katika kundi la waliofuata
mkumbo na kujiingiza katika shiriki kwa kuacha maasi na kufanya mema kwa
ajili ya Ramadhani na siyo kwa ajili ya Allah. Kumbuka kama ulikuwa
unafanya Ibada kwa ajili ya Allah basi yeye yupo na ataendelea kuwapo
daima. Lakini kama ulikuwa unafanya ibada kwa ajili ya mwezi wa
Ramadhani basi tayari umeshaondoka na utajiingiza katika kundi la
washirikina. Allah akulinde na sifa hiyo mbaya.
Miongoni mwa mambo ambayo ni muhimu kwa Muislamu
kuyafanya siku ya Idd kama yalivyofanywa na kusisitizwa na Kiongozi wa
Umma, Mtume Muhammad (S.A.W) ni kutoa zakatul fitri na kupata kifungua
kinywa kabla ya kuswali swala maalumu ya Idd, kubadili njia wakati wa
kwenda au kurudi kuswali Idd, kuswali Idd viwanjani na siyo msikitini.
Pia muhimu zaidi baada ya Idd ni kufunga siku sita
katika mwezi huu wa mfunguo mosi kama tulivyozoea kuiita, aidha kwa
kuzifuatisha au kuzitofautisha katika makumi ya mwezi huu.
Amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake.
“Mwenye kufunga ramadhani na akafuatisha siku sita baada ya Ramadhani,
thamani yake ni sawa na aliyefunga mwaka mzima”. Je wewe huzitaki kheri
na faida hizo za kufunga siku sita za baada ya Ramadhani? Uzisikose
basi.
Kila Muislamu anapaswa kuweka akilini kwamba
Sikukuu ya Idd ni siku ya kutubia na siyo kutibua, ni siku kushukuru na
siyo kukufuru, ni siku ya kuhurumiana na siyo ya kutesana kwa uadui, ni
siku ya kupendana kwa ajili ya Allah na siyo ya kuchukiana, ni siku ya
kutembeleana na siyo ya kukimbiana, ni siku kusalimiana na kujuliana
hali na siyo ya kutukanana, ni siku ya kusuluhishana migogoro na siyo ya
kufufua na kuanzisha migogoro mipya au kugombana, naam ni siku ya
furaha na kuombeana kheri na siyo mabaya.
Neno zuri la kumwambia mwenzako siku ya Idd,
‘Takabbala Llahu Minny Waminkumu Sswiyaam ‘Allah azikubali swaumu zangu
na zenu pia’
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment