Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi,
akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya IPP
jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na kuvamiwa na kuuawa kwa Mapambano
Mashili, mume wa mlemavu wa ngozi, Suzane Mungy, wakati akijaribu
kumuokoa alipovamiwa na watu waliokuwa wakimkata mapanga katika kijiji
cha Buhelele kata ya Nsimbo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora juzi. IPP
itatoa Sh. milioni 10 kwa atakayewezesha kukamatwa kwa waliotenda
uhalifu huo na pia itawasomesha watoto wa marehemu. Kulia ni Gamario
Mboya, kutoka shirika la Under The Same Sun (UTSS), na kushoto ni Katibu
Mkuu wa Chama cha Walemavu wa Ngozi nchini, Ziada Nsemo. PICHA: KHALFAN
SAID
Pia ameahidi kubeba jukumu la kuwasomesha watoto wawili wa Suzan, ambaye mumewe, Mapambo Mashili, aliuawa kikatili kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe (Suzan) asikatwe mkono wake na watu hao katika tukio hilo.
Katika tukio hilo, watoto hao wawili wameripotiwa pia kujeruhiwa na kulazwa hospitali.
Dk. Mengi alisema hayo alipokutana na viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema amefikia uamuzi huo kutokana na kuguswa na uchungu wa madhara yaliyowasibu albino na wengine, ambao wamekuwa ama wakikatwa viungo vya miili yao au kuuawa kabisa kwa sababu ya ulemavu wao.
“Ingekuwaje wewe ni mwanaume na Suzan ni mkeo, au ni mtoto wao, au mdogo wako au ni mtu wako wa karibu? Ungejisikiaje? Niwaachie Watanzania jibu la hilo swali. Tunachukua hatua gani kuwalinda watu hawa. Mtu hachagui, hakuzaliwa wala hakuomba kuwa mlemavu. Mungu hafanyi makosa katika kazi yake,” alisema Dk. Mengi.
Aliongeza: “Uongozi wa Jeshi la Polisi uchukue hatua za haraka hata ikibidi nyumba kwa nyumba wachukue hatua ili liwe fundisho kwa wengine na tuonyeshe kuwa tunawajali hawa wenzetu. Kama kuna mganga amehusika achukuliwe hatua.
Kama kuna mtu anatafuta madaraka achukuliewe hatua kali. Naliomba Jeshi la Polisi Tabora wahusika washikwe, wafikishwe mahakamani ili anayehusika aonje machungu. Aliyetumwa kukata mkono, mganga na kila aliyehusika wote washughulikiwe.”
Alisema yeye hana madaraka ya kuchukua, hivyo atatoa mchango wake kwa kumpa kiasi hicho cha fedha mwananchi yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika na uhalifu huo, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto hao.
Naye Katibu Mkuu wa TAS, Ziada Nsemo, alimshukuru Dk. Mengi akisema ni mtu wa kwanza nchini kuguswa moyoni na kujitokeza hadharani kukemea vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya albino.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment