Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WIZARA ya Afya na
Ustawi wa Jamii imewataka wajasiriamali kuzingatia mchanganyiko wa
vyakula wanavyotumia kutengeneza unga wa lishe kwa watoto chini ya miaka
mitano ili kuepuka athari za kiafya zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza na gazeti
hili kwa njia ya simu Dar es Salaam jana Msemaji wa Wizara hiyo,
Nsachris Mwamwaja alisema kuwa wajasiriamali wengi wamekuwa
wakitengeneza unga huo bila kuzingatia mchanganyiko.
"Wajasiriamali na
wazazi nyumbani wamekuwa wakitengeneza unga wa lishe kwa ajili ya watoto
bila kuzingatia mchanganyiko wa makundi matano matano ya vyakula kitu
ambacho kiafya ni hatari," alisema.
Mwamwaja alisema ni
vema elimu inayotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe
(TFNC) ikazingatiwa kwani taasisi hiyo ina wataalamu wa kutosha na iko
chini ya Wizara ya Afya.
Hivi karibuni katika
maadhimisho ya Siku ya Unyonyeshaji maziwa ya mama,Daktari Bingwa wa
Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Augustine Massawe alisema
unga huo ni hatari kwa sababu mchanganyiko wake si mwafaka kwa watoto.
Dkt. Massawe alisema
utengenezaji wa unga huo hauzingatii vipimo maalumu wala makundi ya
virutubisho anavyopaswa kupata mtoto katika mlo mmoja, ambavyo ni
wanga,protini,vitamini,mafuta na madini.
Alikosoa utengenezwaji wa unga unaochanganywa mahindi, mchele, ulezi, soya, mtama, karanga na dagaa.
"Mchanganyo kama hu
haukubaliki kwa sababu katika mchanganyiko huu wa aina hii kuna orodha
ya nafaka ambazo zina kirutubisho kimoja cha wanga na haziongezi
virutubisho vingine",alisema.
Alipendekeza wazazi kutumia aina moja ya nafaka kama mahindi ambayo yanatoa wanga,mafuta na nyuzi.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment