Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BAADHI ya wakazi mkoani hapa, wamesema kutokana na kuporwa viwanja
na mashamba yao na Halmashauri ya Manispaa, watakihukumu chama tawala
(CCM), kwenye uchaguzi mkuu mwakani kwa kuhamasishana na ndugu zao
kukiangusha mkoani hapa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi zaidi ya 380 kutoka Kata
za Malolo na Ipuli, walisema wameporwa maeneo yao ambayo walikuwa
wakiyatumia kwa kuyaendeleza miaka mingi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa kamati ya migogoro ya
ardhi na mashamba Kata ya Malolo, Robert Jilala, alisema migogoro ya
ardhi ilianza mwaka 2011 baada ya watumishi wa Idara ya Ardhi na
Mipango Miji Halmashauri ya Manispaa Tabora, kufika kwenye maeneo yao
na kuwataka kusitisha kazi walizokuwa wanafanya.
Jilala, alisema walikuwa wakiyaendeleza maeneo yao kwa kulima mazao,
ujenzi wa nyumba na walijulishwa maeneo hayo yatapimwa ili kuendeleza
mji na wao watalipwa fidia.
Alisema watumishi wa Idara ya Ardhi walipomaliza kupima maeneo yao,
walibadilishiwa lugha kwa kuelezwa upimaji uliofanyika ni mradi wa
Manispaa, hivyo kila mwananchi mwenye eneo ama shamba atalipwa fidia ya
fedha.
Alifafanua kuwa walijulishwa na watu wa ardhi kuwa, kila mita moja ya mraba watalipwa sh 150.
Jilala, alisema walipoomba wapimiwe ili wakabidhiwe maeneo yao
walielezwa watalazimka kuyanunua kwa kati ya sh 2,000 hadi sh 2,800 kwa
mita moja za mraba, hali ambayo iliwashangazwa na kuona haki yao
inaporwa.
Aidha, mkazi mwingine wa Kata ya Ng`ambo, Said Juma, alisema alikuwa
na ekari moja eneo la Mbirani, lakini ameambulia hundi ya sh 108,000
ambayo amelipwa mwaka 2013 kupitia benki ya NMB huku baadhi ya wenzake
wakilipwa sh 50,000 na sh 80,000 kupitia hundi zao.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mpera Kata ya Ipuli, Aziz
Kitamanwa, alisema binafsi amedhulumiwa kwa kulipwa hundi ya sh 105,000
ambazo zimelipwa kutokana na eneo lake la zaidi ya ekari moja.
Wananchi hao, wametishia kuishughulikia CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao kutokana na dhuluma waliyofanyiwa.
“Hasira zetu tutazionyesha kwenye uchaguzi mkuu na hatuna ugomvi na
CCM, bali watumishi walioajiriwa na hiyo Serikali ya CCM…tumeumizwa
sana haki zetu kuporwa, tutahamasishana tu kuiumiza,” walisema.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora,
Ghulamdewji Remtulah, alisema fidia zote zilizolipwa kwa wenye viwanja
ni stahiki, huku Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Sipola Liana,
akidai yeye ni mgeni ana mwezi mmoja Tabora hivyo hajui chochote.
Chanzo; Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment