Home » » KIGWANGALA: UWAZIRI SI KIGEZO CHA KUWA RAIS 2015

KIGWANGALA: UWAZIRI SI KIGEZO CHA KUWA RAIS 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla ni mmoja kati ya makada vijana wa chama tawala waliotangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Mbali na Kigwangalla, vijana wengine walioonyesha nia ya kuwania urais ni January Makamba, Mwigulu Nchemba na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, Dk Kigwangalla anasema kuwa waziri si kigezo cha mtu kupewa nafasi ya kugombea urais.
Anasema nafasi hiyo inataka mtu makini anayetambua anachikifanya, asiyekata tamaa na atakayesimamia anachokiamini hadi mwisho wake.
Swali: Tanzania inahitaji rais wa aina gani, je, umri na uzoefu ni kigezo sahihi cha urais?
Jibu: Si lazima uwe na uzoefu wa kutisha ndiyo uweze kuwa kiongozi. Uongozi ni kazi inayohitaji mtu ambaye anajua anachokifanya na ni vyema watu wakamhoji mtu na kujua jambo zuri analotaka kulifanyia taifa lake.
Wanaotaka urais wahojiwe wana kitu gani cha kulifanyia taifa. Mimi nisingefika hapa nilipo kama ningekuwa mtu wa kukata tamaa.
Nimeishi maisha duni na kusoma shule zisizo na walimu wa kutosha lakini nikafaulu na kuingia mtaani ambapo pia nilidai haki yangu kwa kugoma.
Mtu asitazamwe kwa kujenga shule na barabara, inatakiwa utazamwe uwezo wako wa kuvumilia mambo na jinsi asivyotetereka hadi anafanikisha jambo husika.
Wapo walioanza kuwa walimu mpaka kuwa mawaziri na kuanzisha biashara zao mpaka kuwa matajiri wakubwa.
Wapo wenye uwezo wa kuendeleza mambo waliyoyakuta na wapo wenye uwezo wa kuanzisha mambo mapya na kuyasimamia hadi yanafanikiwa.
Swali: Kama CCM isipokuteua kugombea urais au ubunge katika jimbo la Nzega utahamia chama kingine ili ugombee?
Jibu: Sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa zaidi ya CCM. Nilijiunga CCM mwaka 1993 nikiwa kidato cha tatu na nimelelewa katika mfumo wa chama hiki na mapenzi yangu yapo moyoni si kwa lengo la kutafuta madaraka.
Ningekuwa na lengo la kutafuta madaraka ningekwenda upinzani. 2005 niligombea ubunge jimbo la Nzega lakini nilishindwa katika kura ya maoni na vyama vya upinzani viliniomba nijiunge navyo lakini nilikataa.
Nikikosa ubunge na urais siwezi kuhamia chama kingine ili nipate moja ya nafasi hizo, sitakuwa sahihi na siwezi kufanya hivyo kwa sababu naamini katika itikadi za CCM na katika uwekezaji katika siasa ambao hufanyika kwa muda mrefu, unaweza usipate leo urais au ubunge lakini ukapata siku nyingine.
Swali: Unadhani CCM ni chama sahihi kutoa rais mwaka 2015?
Jibu: Sioni rais kutoka chama kingine chochote kile zaidi ya CCM na hakuna uwezekano huo kwa mwaka 2015. Sioni watu makini wanaoutaka urais kutoka nje ya CCM, siyo kama na watusi wengine lakini huo ndiyo mtazamo wangu.
Hatuwezi kupata rais kutoka chama chochote kile cha upinzani kwa sasa.
Ndani ya CCM sina hakika nani atateuliwa kugombea urais lakini ninaamini chama hiki ndiyo kitatoa rais. Kuteuliwa na CCM kugombea urais ni mtihani mzito na ni ngumu sana kupata fursa hiyo.
Kati ya tuliotangaza nia ya kutaka kugombea urais, hakuna hata mtu mmoja ana walau asilimia 30 kwamba atateuliwa ijapokuwa wanaweza kuweka vigezo kwamba kati ya wagombea watakaoteuliwa na Kamati Kuu, awepo atakayewakilisha sura ya vijana, kina mama, wazee, upande wa pili wa muungano (Zanzibar) na sura ya kiitifaki.
Swali: Kati ya urais na ubunge unataka nini zaidi?
Jibu: Hilo liko wazi, sijatangaza nia ya kugombea ubunge lakini kuna uwezekano mkubwa nikarudi kugombea ubunge kama nitakosa fursa ya kuteuliwa na chama kugombea urais.
Sababu ni moja, kwamba nimeshatangaza nia ya kugombea urais na nimetokana na ubunge na watu wamenijua kupitia ubunge, siwezi kukubali kutoka bungeni.
Kukosa urais si mwisho wa maisha au kugombea na kinachotakiwa hapo ni subira tu. Umri unaniruhusu na kama Mungu akinipa uhai nina kila sababu ya kuvumilia na kujipanga ili nikikosa nijipande kugombea wakati mwingine
Ukikosa ni vyema kimkakati kubaki bungeni ili uendelee kuwasemea wananchi wanyonge na kutoa mawazo yatakayosaidia kulisaidia taifa letu.
Swali: Ukipata fursa ya kuzungumza na Watanzania utawaeleza nini kuhusu mchakato wa Katiba?
Jibu: Kama kweli tungekuwa hatulengi kwenye masilahi binafsi ya kisiasa tulikuwa na kila sababu ya kumaliza huu mchakato.
Ukiwa mwana mabadiliko sehemu pekee unayoweza kufanya mabadiliko ya namna nchi inavyoendeshwa kwenye taifa lolote lile ni kwenye Katiba.
Ukipata fursa ya kuwa kwenye mchakato wa Katiba na kama nchi ipo makini na inataka kupata Katiba nzuri ni vyema mkaitumia fursa hiyo kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo.
Kila siku kikazi chetu kinasema kuwa mfumo ni mbovu na watu wengi wanadhani tatizo ni CCM kumbe siyo sahihi.
Inawezekana mfumo wa kisheria ukawa na tatizo na mfumo huu wa sheria unaanzia kwenye sheria mama ambayo ni Katiba.
Hata mbadilishe sheria zote, lakini kama hamjabadilisha sheria mama lazima mtakwama tu sehemu.
Nimetangaza nia ya kugombea urais, ningependa tuwe tumemaliza mchakato wa Katiba kabla sijawa rais ili tuwe tumeweka mfumo mpya wa sheria ili nikija kuwa rais niongoze kwa kutumia mfumo mpya.
Kuna mambo yanafanyika sasa na unaweza kuilaumu CCM kama chama kinachounda sera, ukamlaumu rais, mawaziri na wabunge wanaotokana na CCM , kumbe lawama si zao na wanashindwa kufanya kazi kutokana na uwepo wa mfumo mbovu. Hii ndiyo fursa pekee ya kuondoa mfumo mbovu na kuweka mfumo mpya. Mfano, muingiliano wa kiutendaji kati ya makatibu wakuu na mawaziri.
Unaweza kumlaumu waziri kumbe makosa ni ya Katibu Mkuu maana katika wizara, waziri hana sauti.
Hata mbunge, anatakiwa kubanwa kama atashindwa kuisimamia serikali, lakini wananchi wanamhoji mbunge unataka tukupe ubunge umefanya nini. Mbunge ni msemaji tu ili anachokisema kitekelezwe na serikali.
Tunapenda sana kupiga kelele na tunakataa ukweli kwamba muda wa miaka miwili ulikuwa hautoshi kuandika Katiba, tulihitaji muda zaidi. Sisi kwa sababu tunaogopana tunashindwa kusema kuwa serikali iliyopo madarakani iongezewe muda ili kumaliza mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa sababu mwaka 2016 ambao tunataka mchakato huu uendelee tutakuwa na rais mpya na asilimia 70 ya wabunge wapya.
Itabidi kabla ya wananchi kuanza kupiga kura ya maoni wananchi watatakiwa kuhamasishwa na vyama vya siasa na wabunge wao kwa sababu wanajua sababu za wao kupitisha ibara mbalimbali za rasimu ya Katiba. Kama asilimia 70 wataondoka na kuwa na rais mpya kazi itakuwa ngumu katika zoezi hilo.
Swali: Unafikiri ni sahihi kwa wanaosema kuwa CCM ina mtandao mpana wa rushwa na ndiyo maana kinashinda katika chaguzi?
Jibu: Siyo kweli. Unajua CCM ni chama chenye mtandao mkubwa kuanzia katika ngazi ya mtaa hadi taifa.Wakati nagombea Nzega niliishiwa fedha kabisa lakini rafiki zangu walinichangia nikashinda. uchaguzi. Sasa hilo huwezi kusema kuwa ni rushwa.
Nilishinda Ubunge kwasababu ya mtandao wa chama na sera zake nzuri ambazo wananchi wanaziunga mkono.
Nilikuwa miongoni mwa wana-CCM walioshiriki katika kampeni za ubunge jimbo la Igunga. Kuna vyama vilipita mitaani na kutoa fedha kwa wapigakura, sisi hatukutoa hata senti moja lakini mgombea wetu alishinda. Hiyo ni kwasababu ya mtandao mzuri wa chama.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa