Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Dk. John Magufuli
Abiria
zaidi ya 100 wanaokwenda mikoa ya Tabora na Kigoma wanaotumia usafiri
wa treni wamekwama jijini Dar es Salaam kwa siku mbili baada ya Kampuni
ya Reli nchini (TRL) kusitisha safari bila taarifa.
Abiria hao wengi wao wanawake na watoto, wamesema wanakabiliwa na
hali mbaya ya kukosa chakula na huduma ya choo na kuhatarisha maisha
yao.
Akiongea mmoja wa abiria hao Laurent Mayee (51) mkazi wa Kigoma,
alisema treni hiyo ilitakiwa kuanza safari juzi saa 11: 00 jioni lakini
hadi jana saa 8 mchana hawajaondoka na hakuna kiongozi aliyejitokeza
kutoa ufafanuzi.
Alisema yeye na ndugu yake ambaye ni mgonjwa walilipia Sh. 55,400
kila mmoja kwa behewa la daraja la pili, lakini tangu juzi asubuhi
walipofika kituoni hapo wamejikuta wanasota kusubiri usafiri huo bila
kuwa na uhakika wa lini wataondoka.
Mayee alisema uongozi wa TRL wamekuwa wakibadilisha ratiba kila wakati kupitia ubao wa matangazo.
Alisema ratiba ya kwanza iliyobadilishwa ilionyesha treni hiyo
ingeanza safari saa 4:00 usiku, lakini ulipofika muda huo ilibandikwa
ratiba nyingine ikionyesha safari hiyo imeahirishwa hadi jana saa 4:00
asubuhi.
Hata hivyo ratiba hiyo ilipanguliwa na kueleza safari ingeanza saa
11 jioni huku hakuna ufafanuzi wowote wa sababu za kuahirishwa kwake.
“Tangu tufike hapa jana (juzi) tumekuwa kama tupo gizani, hatujui
lini treni itaondoka kitu kibaya zaidi tupo watu wengi tukiwa hatuna
chakula, hatujui tutaishi vipi kwa siku zote tukiwa hapa,” alisema
Mayee.
Abiria mwingine Hamisa Adamu (20) anayesafiri kwenda Kigoma,
alieleza kwamba shida kubwa wanayokabiliana nayo ni kukosa sehemu ya
kulala na vyoo vya kujisaidia hasa kwa akina mama na watoto ambao
hawana uwezo wa kulipia huduma hiyo.
Hamisa alisema hakuna anayepingana na kuwapo kwa tatizo, lakini
ingetumika busara kwa viongozi kuongea na abiria hao kwa kuwaeleza
tatizo pamoja na kusaidia mahitaji mbalimbali ya muhimu.
“Wewe fikiria mama atapata wapi pesa ya kulipia huduma ya choo
Shilingi 300 ya kila anapohitaji yeye na mtoto wake, huku hajapata
chakula wala maji tunaomba serikali kuingilia kati jambo hili haraka,”
alisema John Daniel (30) ambaye anasafiri na treni hiyo akielekea
Kaliuwa Mkoani Tabora.
Hata hivyo alipotafutwa Ofisa Habari wa kampuni hiyo Midladjy Maez
kwa kutumia simu yake ya mkononi hakuweza kupatikana baada ya kuita bila
kupokelewa.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, alipotakiwa kuzungumzia
suala hilo, alisema hawezi kueleza chochote kwa sababu yupo katika
msafara wa mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment