DSC_0015
Zahara Muhidin Michuzi akiwa nje ya ukumbi wa uchaguzi leo mapema.
Leo hii mchana binti ya mpiga picha na blogger maarufu nchini anayeambatana na rais Kikwete katika ziara zake, Muhidin Issa Michuzi Bi Zahara Michuzi alishindwa kupata kura za kutosha kumwezesha kushinda nafasi ya ubunge wa vijana kupitia tiketi ya CCM mkoa wa Tabora baada ya msanii wa filamu Bi Irene Uwoya kupata kura 34 kati ya 39 zilizopigwa.
Zahara ambaye ni mhitimu wa shahada ya uchumi toka chuo kikuu cha UDOM aliyakubali matokeo hayo bila kinyongo  na kusema “Napenda kuwashukuru wagombea wenzangu na wajumbe wote, pamoja na kura mlizonipigia hazikutosha leo lakini nitabaki na azma yangu ya kuwatumikia wana Tabora” wajumbe walimshangilia sana na kumpongeza kwa ukomavu wa kisiasa aliouonesha ambapo mwenzie Mariam Shamte alisusia na kuondoka ukumbini. Mariam alimteua nduguye Hapsa kumwakilisha ktk uhesabuji kura hizo ambazo yeye Mariam alipata kura 3. Hakuingia ukumbini katika usomwaji wa matokeo.
Awali mgeni rasmi wa mkitano huo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Bw Hassan Wakasuvi aliwaeleza wajumbe kuwa Obama alizaliwa na baba raia wa Kenya na mama Mmarekani lakini leo hii anaiongoza Marekani, hivyo wasione ajabu kama pana mgombea asiyetokea Tabora kiasilia. Bila shaka alikuwa akimzungumzia Irene Uwoya ambaye kabla ya uchaguzi wakazi wengi wa Tabora walielekea kutomkubali kwa kusema kwa nini CCM ituletee mgombea toka Arusha, Moshi au Dar es Salaam, na kwa nini Irene asigombee Dar anapoishi au Kwao kaskazini? kwani Tabora hakuna vijana wenye uwezo wa kugombea? waliendelea kuhoji kuwa ni vipi Irene atayajua matatizo ya vijana wa Tabora ambao hawajui wala hana uelewa na mkoa huo? Lakini hayawi hayawi hatimaye yamekuwa kwa Irene ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho. Kama maneno ya Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Tabora yalifanya kazi kusababisha Irene Uwoya achaguliwe kwa kishindo mimi na wewe hatujui.