Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
WANANCHI
wa Jimbo la Igulula wilayani Uyui Mkoani Tabora wamepongeza hatua na
jitihada zilizofikiwa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya huduma
za maendeleo ya jamii katika kipindi cha miaka 55 ya uhuru wa Tanzania
Bara.
Wanazitaja
huduma hizo ni pamoja na maji, afya, nishati, na elimu ambazo kwa
kipindi kirefu zilikuwa zikikwamisha maendeleo ya wananchi, na
kukamilika kwake kunahitimisha ndoto za siku nyingi za kupatikana kwa huduma muhimu jimboni humo.
Wakitolea mfano wanasema mwaka 2015 jimbo hilo limepata nishati
ya umeme kupitia gridi ya Taifa kwa asilimia 70 na hivyo kufanya kata
za Goeko, Ngololo, Kigwa na Igalula kupata nishati hiyo adhimu sambamba
na kufikisha umeme wa mwanga wa jua katika kata za Tara, Loya, na Lutende.
Mbunge
wa jimbo la Igalula Athumani Mfutakamba akizungumza na mwandishi wa
habari hii, anaeleza kinagaubaga neema zilizopatikana ndani ya miaka 55
ya Uhuru katika jimbo hilo na kukiri wazi zinamfanya awe na shauku ya
kuhadithia kila mara.
Dkt.
Mfutakamba anasema jitihada hizo za Serikali pamoja na wadau wengine za
kufikisha umeme katika jimbo la Igalula imekua nyenzo muhimu kwa uchumi na ustawi wa maendeleo ya jimbo hilo.
“Umeme huu umekua ukitumika si tu kuwashia taa ama kumulika majumbani na mitaani ila hutumika pia hospitalini, shuleni na katika shughuli mbalimbali zinazotumia nishati hiyo” anasema Dkt Mfutakamba.
Kwa
mujibu wa Dkt. Mfutakamba anasema jimbo hilo limepata mafanikio makubwa
katika sekta ya maji kwa kujenga visima virefu viwili vilivyoweza
kutatua matatizo ya maji katika jimbo hilo.
Dkt.
Mfutakamaba alisema jimbo hilo pia limefanikiwa kukamilisha ujenzi wa
zahanati za Imalaseko, Goeko, Ngololo, Igalula na Loya pamoja na kupata
vitanda ambavyo vinatumika kusaidia wanawake wanaojifungua.
Kuhusu
sekta ya elimu, Mbunge Mfutakamba alisema kwa miaka mingi jimbo hilo
halikuwa na shule ya sekondari, ambapo hadi sasa jimbo limeweza kuwa na
shule ya sekondari Goeko.
Sambamba
na hayo, Mbunge huyo aliipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na
Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo za kusimamia kikamilifu rasilimali
fedha na watu.
“Ni
lazima tuunge mkono jitihada hizo kwa kulipa kodi ili fedha
zitakazopatikana zisaidie katika shughuli mbalimbali za kutuletea
maendeleo, badala ya kutegemea wafadhili pekee” alisema Mbunge huyo.
mwisho
0 comments:
Post a Comment