Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Serikali
ya Kuwait imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola
za Kimarekani milioni 34 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 74.8 kwa
ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 85 kwa kiwango cha
lami kutoka eneo la Chaya hadi Nyahua mkoani Tabora.
Ahadi
hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na mwakilishi wa Balozi wa Kuwait
hapa nchini, Bw. Mohammad Rashid Alamiri, aliyeongoza ujumbe kutoka
Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, ulipomtembelea na kufanya mazungumzo na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ambapo wamejadili
masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya
Tanzania na Kuwait.
Dkt.
Mpango ameushukuru Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund) kwa
kuipatia Tanzania mkopo huo wenye masharti nafuu utakaochochea
maendeleo kwa Watanzania hususani wanaoishi katika maeneo ambayo
barabara itajengwa kwa kuwa watarahisishiwa usafiri na usafirishaji wa
bidhaa zao hivyo kukuza uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Amesema
kuwa kipande hicho cha barabara kutoka Chaya hadi Nyahua, ambacho kiko
Barabara Kuu itokayo Dar es salaam kwenda katika mikoa ya Tabora na
Kigoma, licha ya umuhimu wake katika kukuza biashara na usafiri na
usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo inayokwenda nchi jirani,
ilikuwa haijapata fedha kwa ajili ya ujenzi wake.
“Riba
waliyoiweka mezani kwa mazungumzo ni asilimia 2 lakini nimewaomba
waangalie uwezekano wa kuiteremsha walau ifike asilimia 1.5 na
wamependekeza kipindi cha kuanza kulipa mkopo kiwe miaka ishirini ijayo
lakini nimewaomba wasogeze hadi kufikia miaka 25 kama ilivyo kwa mradi
wa Hospitali ya Mnazimmoja” aliongeza Dkt. Mpango
Dkt.
Mpango amesema Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wake huo wa Maendeleo
wameonesha nia ya kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi
na ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyoko Visiwani Zanzibar.
“Nawahakikishia
kuwa baada ya muda si mrefu wananchi wa mikoa ya Tabora na Kigoma
watarajie kuona mkandarasi akiingia kazini ili kujenga barabara hii
muhimu sana kwao na kwa uchumi wa Taifa kwa ujumla” Alisisitiza Dkt.
Mpango.
Ameeleza kuwa ujenzi wa kipande cha barabara hiyo kutoka Chaya hadi Nyahua unatarajia
kugharimu shilingi Bilioni 61 lakini Kuwait haitatoa fedha zote hivyo
ameuomba Mfuko huo uangalie uwezekano wa kutoa kiasi hicho chote cha
fedha ili uweze kukamilika mapema.
0 comments:
Post a Comment