MKAZI wa Kata ya Chemchem katika Manispaa ya Tabora, Asha Kayamba
amemuonba Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na vyombo vya ulinzi na
usalama vimsaidie ili askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliompiga
mwanawe na kumsababishia kifo wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika barua yake, amemlalamikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
kuwaachilia askari tisa wa Kikosi cha 823 JKT Msange kwa madai ya
kukosekana ushahidi.
Asha katika barua hiyo ya Desemba 19, 2015, alisema anasikitika kuona
haki yake inapokonywa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba
kijana wake Omary Zuberi Shaban (19) ambaye sasa ni marehemu, aliuawa na
wananchi wenye hasira.
“Kwa kweli nilipatwa na mshtuko mkubwa sana baada ya kuona haki yangu
inapokonywa kwa kisingizio cha mtoto wangu kuuawa na watu wenye
hasira,” alieleza Asha katika barua yake kwa DPP.
Alibainisha kuwa mwanawe alishambuliwa na wanajeshi hao (majina na
vyeo vyao tunayahifadhi) mchana na wala wananchi hawakuhusika katika
tukio hilo kwani wao walikuwa ni watazamaji tu.
Alisema mwanaye alipigwa na askari hao Septemba 10, mwaka jana na
alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete kwa siku nne hadi alipoaga
dunia Septemba 13, 2016 saa tano usiku.
Barua hiyo ilieleza kuwa Polisi ilifanya upelelezi wa tukio hilo na
kuwatia nguvuni watuhumiwa tisa wakati mama wa marehemu, Regina Masuva,
kijana aliyenusurika Zuberi Haruna, Mwaka Zuberi (mama mzazi wa Zuberi)
na watu wengine walitoa maelezo kuhusu tukio hilo.
Alifafanua kuwa Septemba 20, 2016 watuhumiwa wa mauaji ya mwanawe
ambao ni askari tisa wa Kikosi cha 823 Msange JKT walifikishwa
mahakamani na kusomewa mashtaka na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Samson
Kabigi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Agatha Chugulu.
“Baada ya kusomewa mashitaka hayo, kesi hiyo ilipangwa kutajwa Oktoba
13, 2016 na Oktoba 28, 2016. Lakini siku hiyo watuhumiwa hao
hawakufikishwa mahakamani.
“Nilipohoji kwa nini nilijibiwa kuwa walifanya fujo ndani ya mahabusu
ya gereza la Uyui mjini Tabora, jambo lililowafanya wapewe adhabu hivyo
hawataweza kufika,” alieleza mama huyo katika barua hiyo.
Alisema shauri hilo lilipangwa kutajwa Novemba 10, mwaka huu,
nilipofika siku hiyo watuhumiwa walikuwepo mahakamani ambapo kesi yao
ilipangwa kutajwa tena tarehe 24 Novemba, mwaka huu.
Alisema kuwa utata ndio ulianzia hapo.
Alidai kuwa kabla ya kufika tarehe hiyo, watuhumiwa wote tisa
walionekana mtaani jambo ambalo lilimpa mshituko mkubwa na kufanya
afuatilie mahakamani, Polisi na Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali mjini
Tabora bila kupata majibu muafaka.
Alidai alipofika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali, alikutana na ofisa
aliyemtaja kwa majina ya Jackson Bulashi ambaye alidai kuwa alimjibu
kwamba watuhumiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na shauri la mauaji,
wameachiwa kwa kuwa hakuna ushahidi wa kujitosheleza.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment