Home » » TABORA YASHIKA NAFASI YA 10 S/MSINGI KITAIFA

TABORA YASHIKA NAFASI YA 10 S/MSINGI KITAIFA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Judith Mhina – Maelezo

Mkoa wa Tabora umeonyesha maajabu sekta ya Elimu baada ya kushika nafasi 10 kimkoa kitaifa 2016.

Akiongea kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Tabora Bw Emmanuel Malima alisema: “ Ukiangalia mwenendo wa ufaulu kwa Mkoa ulikuwa hauridhishi tangu 2013 ufaulu ulikuwa wastani wa 34.5 na kushika nafasi ya 25 kitaifa ambayo ni ya mwisho, 2014 ufaulu 42.09 nafasi ya 23 2015 ufaulu 50.5 nafasi ya 25 na 2016  ufaulu 71.35 nafasi ya 10 kitaifa, hii imetupa heshima kubwa baada ya kukaa namba za mwisho kwa miaka mitatu mfululizo”.

Akidhibitisha juu ya ufaulu huo,  Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa Bw Emmanuel Malima alieleza : “Matokeo hayo yametokana na juhudi na ushirikiano katika masuala muhimu yaliyoainishwa na Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu yaani EQUIP- Tanzania, katika kuimarisha utendaji wa waalimu, kuimarisha uongozi wa shule, kuimarisha utendaji wa Elimu katika Wilaya na kuongeza ushiriki wa jamii  kuboresha elimu yaani kujizatiti katika - K4. 

Aidha, Bw Malima aliyasema hayo wakati wa Warsha ya kuimarisha mawasiliano au utoaji wa taarifa katika sekta ya Elimu chini ya Mpango wa Kuinua Elimu EQUIP Tanzania, yaliyofanyika mwezi Novemba katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa takriban siku 6. Mawasiliano au taarifa hizo zinatoka ngazi ya shule, jamii vijijini kata hadi Wilaya.

Bw Malima alieleza jinsi K4 zilivyoweza kubadili mazoea ya utendaji katika shule za msingi na kuleta mabadiliko makubwa katika Mkoa mzima wa Tabora ambao katika siku za nyuma Mkoa ulikuwa maarufu sana katika suala zima la elimu.

Mpango wa Kuinua Elimu Tanzania EQUIP-T ulianzishwa mwaka 2014 na una vipengele vitano ambavyo ni: Kuwawezesha Walimu katika kuimarisha mbinu za stadi za ufundishaji, Kuboresha uongozi wa Walimu wakuu na wasaidizi wao, Kusaidia utendaji wao wa kazi na uongozi wa shule;  Kujenga uwezo wa Maafisa Elimu kuongoza kwa ufanisi, kusimamia elimu na mfumo wake; Kuimarisha Ushiriki wa Jamii  Wazazi na Viongozi wa vijiji na mitaa ili kuleta maendeleo ya shule Elimu ya Kujitegemea; na Kuboresha  mifumo ya ukusanyaji , utumiaji na utoaji wa taarifa za kielimu.


 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa