Na Tiganya Vincent
Tabora
29.5.2017
Katibu
Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara amewaagiza Wakurugenzi wote wa
Manispaa na Halmashauri mkoani humo kuhakikisha wanawaondoa haraka watu
waliovamia maeneo ya Taasisi na Shule na kujenga makazi yao.
Dkt. Ntara alitoa agizo hilo jana mjini Tabora wakati wa kikao na watendaji mbalimbali wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Alisema
kuwa haiwezekana hadi hivi sasa watu waendelee kuishi katika maeneo ya
Shule na Wakurugenzi Watendaji wamekaa kimya bila kuchukua hatua yoyote.
Aidha,
Dkt. Ntara alisema kuwa zoezi la kuwaondoa wavamizi hao ni vema
likaenda sanjari ya ujenzi wa uzio unazunguka eneo la shule husika ili
kuzuia watu ambao watakuwa wameondoka kwa hiari na wale watakalazimishwa
kuondoka kuweza kurejea tena.
Aliongeza
kuwa ujenzi wa uzio huo sio lazima uwe wa gharama kubwa kwani wanaweza
kutumia mbinu ya kupanda miti kuzunguka eneo la taasisi au shule husika kama ulinzi na kuonyesha miapaka ya eneo husika.
Aidha
,Dkt. Ntara alisisitiza kuwa wakati ukarabati wa shule kongwe kama vile
Shule ya Wavulana na Wasichana za Tabora na Milambo ukitarajia kuanza
hivi karibuni ni vema Wakurugenzi wakahakikisha maeneo ya shule hizo na
nyingine wavamizi wameondoka.
Aliongeza
kuwa uvamizi huo umesababisha wanafunzi na wanavyuo kukosa hata maeneo
ya kuendesha elimu ya michezo kwa ajili ya maandalizi ya wataalam wa
baadaye wa sekta hiyo.
Dkt Ntara alisema kuwa kuanzia sasa Watendaji wapite katika kila shule zilizovamiwa na kuweka alama za X katika nyumba zilizojengwa katika shule.
0 comments:
Post a Comment