Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akisaini kitabu kitabu cha wageni chuoni hapo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza na uongozi wa chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora BTI alipotembelea chuoni hapo leo. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho Semu Daudi na Mratibu Mkuu wa Mafunzo, Igunda John.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati akitoa maelekezo mbalimbali chuoni hapo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry baada ya kutembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora, BTI leo.
NA HAMZA TEMBA - WMU
-----------------------------------------------------------
Waziri wa Maliasili na
Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry kutumia fursa ya uwepo wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora, BTI mkoani humo kwa kuandaa utaratibu maalum utakaowawezesha wananchi hususan wafugaji wa
nyuki kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji wa nyuki chuoni hapo kwa
ajili ya kuboresha uzalishaji wa bidhaa hiyo na kuwaongezea kipato.
Waziri Maghembe ametoa
kauli hiyo leo alipotembelea chuoni hapo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya
siku mbili Mkoani Tabora kwa ajili kujionea changamoto mbalimbali za uhifadhi na
kuona namna kukabiliana nazo ikiwa ni ahadi aliyoitoa bungeni wakati
akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara
yake kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.
“Mkuu wa Mkoa, tafadhali andaa
utaratibu maalum kwa wananchi wako, wale wafugaji wa nyuki wanaweza kuja kwenye
chuo chetu hapa hata siku tatu, hata siku mbili, wafundishwe namna bora ya kufuga
nyuki, yani watoke kabisa huko Skonge, waletwe hapa, walale hapa sku moja au
mbili wafundishwe baadae warudi makwao wajue namna bora ya kufuga na kuvuna
asali,” alisema Maghembe.
Kwa upande wake Mkuu huyo
wa Mkoa wa Tabora alisema maelekezo hayo kwao ni faraja kwakuwa tayari kuna
maelekezo ya kiserikali kusaidia makundi ya kinamama na vijana ikiwemo utoaji
wa mikopo kwa vikundi vyao vya ujasiriamali.
“Katika Mkoa wangu tuna makundi haya ya kinamama
na vijana ambao tumetakiwa kuwasaidia kwa maana ya kutenga “percent” (asilimia)
fulani katika “own source” (vyanzo vya ndani vya mapato), kwahiyo kwa maelekezo
hayo hayo nitakachofanya mimi ni kuhakikisha kwamba tunaenda kuwaeleza katika
hali ya kawaida kwamba tungeweza kuwapa mikopo lakini tungependa tuwape mikopo
baada ya kupata taaluma na waweze kujua vizuri namna bora ya kufuga nyuki na kurina
asali”, alisema Mwanri.
Mkuu wa Chuo hicho, Semu
Daudi alisema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 155 na kinatoa mafunzo ya Cheti
na Diploma ya Ufugaji wa Nyuki.
Naye Mkuu wa Kituo kidogo
cha Utafiti wa Ufugaji Nyuki chuoni hapo, Humphrey Natali alisema kituo hicho
kinakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi ikiwemo usafiria ambapo gari lililokuwepo
limepelekwa matengenezo na kompyuta zilizopo nazo ni za muda mrefu.
Waziri Maghembe ameahidi kukipatia kituo hicho gari moja huku akimuagiza, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo kuona uwezekano wa kumaliza
changamoto mbalimbali chuoni hapo.
0 comments:
Post a Comment