RAIS John Magufuli ameagiza watu waliojenga kwenye hifadhi ya
barabara na reli, nyumba zao zibomolewe kwani sheria lazima isimamiwe,
na kuagiza zianze za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao
wanagoma zisibomolewe.
Aidha, amebainisha kuwa ni mateso kuwa waziri chini ya utawala wake
kwa sababu inawabidi mawaziri hao saa nyingine kushiriki mateso ambayo
yeye anayapata hasa linapokuja suala la kuhakikisha wananchi wanapata
maisha bora. “Nasikia kuna baadhi ya watu, tena wanaCCM wanawaambia eti
msibomoe, mimi naagiza bomoeni zote na tena anzeni na nyumba za
wanaCCM,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua barabara ya Kaliua –
Kazilambwa iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 61 umefanyika siku ya kwanza
ya ziara ya Rais Magufuli mkoani Tabora baada ya kukamilisha ziara yake
mkoani Kigoma mapema jana.
Aidha, amempa mwezi mmoja Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha kuwa barabara inayounganisha Kaliua
na Urambo yenye urefu wa kilometa 28 inajengwa kwa kiwango cha lami.
Mbali na barabara hiyo ya Kaliua – Urambo, Rais Magufuli pia alimwagiza
Profesa Mbarawa kuhakikisha ndani ya siku 45 anampata mkandarasi wa
kujenga barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85 kwa kuwa
fedha za barabara hiyo zipo tayari.
Rais Magufuli alisema wananchi wa Tabora wameteseka kwa muda mrefu
kwa kukosa barabara bora, hivyo chini ya serikali yake ni lazima
barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami na kwa ubora unaotakiwa.
“Kuongoza nchi inabidi kuwa mkorofi kidogo, ndiyo maana natoa maagizo
haya hadharani, siwanyanyasi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Ninawaamini ndiyo maana natoa maagizo hayo, nisingewaamini
nisingeagiza, mnafanya kazi nzuri.”
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya wananchi wa Tabora kuharibu misitu
na kusababisha ukame, akisema watu wanakata miti ovyo kwa kuchoma mkaa
na wengine kulisha mifugo hali inayosababisha maji kukauka na nyuki
kukimbia. Alisema Tabora na kwa namna ya pekee Kaliua kulikuwa na
hifadhi nzuri ya mazingira, lakini uharibifu wa mazingira umesababisha
uzalishaji wa asali bora duniani kutoka Tabora kupungua.
“Mnafyeka mapori na kukata miti ambayo mingine iliishi zaidi ya miaka
150, halafu anayekata huo mti ana umri wa miaka 20, lakini wafugaji pia
mnatakiwa kufuga kisasa kwa kupunguza idadi ya mifugo, msifuge bila
mipango, nampongeza Mkuu wa Wilaya ya hapa kwa kupiga marufuku uharibifu
wa hifadhi,” alisema Rais Magufuli. Akijibu hoja zilizotolewa na
wananchi kuhusu zao la tumbuku mkoani humo, Dk Magufuli alisema kulikuwa
na makosa yaliyofanywa na serikali na makosa yaliyofanywa na wananchi
wenyewe.
Akifafanua hoja hiyo, Rais Magufuli alisema serikali ilifanya makosa
kwa kuruhusu kuwepo kwa tozo nyingi kwenye mazao. Alisema tozo hizo
zilisababisha kushuka bei kwa mazao hayo na kuwasumbua wananchi. Alisema
kulikuwa na tozo zaidi ya 30 kwenye zao la kahawa, lakini serikali yake
imejitahidi kuziondoa tozo 80 kwenye sekta ya kilimo.
“Lakini pia wananchi waliokopeshwa pembejeo kama mbolea na dawa
kutoka kwenye vyama vya ushirika, hawakurudi kuuza mazao yao kwenye
ushirika walikokopa fedha, walikwenda kuuza kwingine; lakini hata
viongozi wa ushirika mliowachagua wengi walikuwa mchwa, walafi na
majizi, hatukujenga ushirika imara,” alieleza Rais Magufuli katika
hotuba zake zilizorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Aliongeza kuwa alimwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatilia
matatizo ya tumbaku mkoani Tabora na atakapokamilisha kazi hiyo,
ufumbuzi utapatikana, hivyo akawataka wananchi wawe wavumilivu. Aidha,
aliwataka wananchi wa Kaliua kumpa ushirikiano mbunge wao, Magdalena
Sakaya wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuwa anasimamia maendeleo ya
wananchi.
Alisema maendeleo hayana chama na ni mara kumi uwe na mbunge wa CUF
au chama kingine anayetekeleza mambo ya CCM kuliko kuwa na mbunge wa CCM
anayetekeleza mambo ya vyama vingine. Akiwa mjini Urambo jana jioni, Dk
Magufuli aliweka wazi kuwa ni mateso kuwa waziri chini ya utawala wake
kwa sababu inawabidi mawaziri hao saa nyingine kushiriki mateso ambayo
yeye anayapata hasa linapokuja suala la kuhakikisha wananchi wanapata
maisha bora.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara alipokwenda
kufungua barabara ya Urambo – Tabora yenye urefu wa kilometa 64
iliyojengwa kwa fedha za ndani Sh bilioni 118, Dk Magufuli alisema
mawaziri wake ni lazima watambue hilo, lakini pia anashukuru kwamba wote
wanafanya kazi nzuri. Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani
Afrika zinazojenga barabara zake kwa kutumia fedha zao wenyewe. Aidha,
amewasisitiza wananchi kulipa kodi kwani ndiyo inayotumika kuleta
maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, elimu bure, maji na afya.
Amewataka wananchi wamuunge mkono hasa anapopambana na ufisadi kwani
hakuna mtu anayejua siri za nchi kama Rais
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment