Home » » MILAMBO WAOMBA RADHI KWA UTOVU WA NIDHAMU ULIOFANYWA NA WENZAO.

MILAMBO WAOMBA RADHI KWA UTOVU WA NIDHAMU ULIOFANYWA NA WENZAO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Tiganya Vincent
RS TABORA
27 September 2017
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Milambo wameiomba radhi Serikali  kwa vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyosababisha baadhi wamefikishwe Mahakamani na wengine kulazimishwa kuhamishwa shule hiyo kwa makosa kutoroka shuleni nyakati za usiku.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati(PCM) ambaye pia ni Makamu Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule hiyo Baraka Fundo kwa niaba ya wanafunzi wenzake waliobaki shuleni hapo wakati Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alipopita kukagua miradi mbalimbali ya shule.
Alisema kuwa matukio mawili yaliyofanywa na wenzao yamechafua jina zuri la Shule hiyo ya Milambo ambayo ina historia ya kuzalisha vijana wengi wanajiunga na vyuo vikuu hapa nchini na kutoa mchango mkubwa katika Taifa hili.

Fundo alisema kuwa wanafunzi waliobaki shuleni ni safi na wako pale kwa ajili ya kusoma na kuendelea mbele zaidi ili waje wasaidie katika kuliendeleza Taifa hilo katika sekta mbalimbali na kwa ajili ya kuunga juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya ujenzi wa viwanda.

“Mkuu wa Mkoa tunaomba radhi kwa matukio yaliyofanywa na wanafunzi wenzetu ya kufanya fujo mitaani na kujeruhi watu  na hatimaye wamefikishwa Mahakamani…na wale waliotoroka usiku na kukutwa kuwa wamelala nje…sisi tuliobaki tunakuahidi kuwa ni wanafunzi safi na hatuwezi kushiriki katika vitendo viovu ili kulinda heshima ya Shule yetu” alisema Fundo.

Alisema kuwa ili kuhakikisha wanaondoa dosari iliyojitokeza kupita wanafunzi wenzao ambao hawapo tena shuleni hapo watajitahidi kufanya vizuri katika mitihani yao ya Kidato cha Sita ijayo ikiwa ni sehemu ya kujutia makosa ya wenzao.
Akizungumza na wanafunzi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri alisema kuwa matukioa yaliyofanywa na baadhi ya wenzao ambao hivi hawapo shuleni hapo  vilitia doa shule hiyo ambayo ina historia nzuri hapa nchini.

Aliwataka wanafunzi ambao wamebaki baada ya kuwaondoa wale waliokuwa na matatizo wazingatie kilichowapeleka Shuleni na taratibu na Sheria za Shule na zile za Nchi ili waweze kutimiza ndoto zao na za wazazi wao.

Mwanri alisema kuwa jambo lolote litakalowafanya washindwe kumaliza masomo yao litakuwa limesababishia hasara Taifa kwa kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi ili kuhakikisha watoto wanasoma na wakuja kuwa wataalamu katika sekta mbalimbali katika ujenzi wa Taifa.

Matukio ya utovu wa nidhami katika Shule hiyo yalitokea hiivi karibuni ambapo yalipelekea wanafunzi 22 kupandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka 12 matano yakiwa ya kujeruhi na saba ya kuharibu mali na wengine 37 wa Shule hiyo walilazimika kuhamia  katika Shule nyingine baada ya kupatikana na kosa la kutoroka Usiku na baadaye kusamemehewa na Bodi  ya Rufaa ya Mkoa huo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa