NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
10 January 2018
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora kimewataka wanafunzi wa Shule za
Msingi na Sekondari kujenga tabia na utamaduni wa kupanda miti ya
matunda na kivuli kwa ajili ya manufaa yao ya siku za usoni.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Igunga na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora
Hassani Wakasuvi wakati aliposhiriki uzinduzi wa upandaji miti kando
kando ya barabara kuuu kutoka Tabora kuelekea Singida uliozinduliwa na
Mkuu wa Mkoa huo Aggrey Mwanri kwa ajili ya wanafunzi hao.
Alisema
kuwa wanafunzi wasione kitendo cha upandaji miti kinachoongozwa na
viongozi wa kuanzia ngazi ya kitaifa kwenda mikoani hadi ngazi za chini
kuwa ni adhabu bali kina manufaa na muhimu katika maisha yao ya baadaye.
Wakasuvi
alisema kuwa ni vema wakafanya utaratibu huo kuwa wakudumu kwa kupanda
miti mbalimbali ikiwemo ya matunda kwa wingi katika maeneo ya mashule na
majumbani ili wapate chakula na kivuli.
“Nawaomba
wanafunzi achene masuala ya ku-chat katika someni sana na pandeni miti
kwa wingi ili mpate kivuli na matunda …na kazi hii msiione kama ni
adhabu bali ni akiba mnayojiwekea kwa ajili yenu na vizazi vyenu”
alisema Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Tabora.
Aidha
Mwenyekiti huyo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa alivyojitokea
katika kuhakikisha kuwa miti inapandwa kwa wingi katika maeneo
mbalimbali ikiwemo katika barabara kuu kwa ajili ya kutaka kuigeuza
Tabora kuwa ya kijani na kurudisha uoto wa asili wa eneo hilo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora alisema kuwa wamekusudia
kuhaklikisha barabara zote zinaingia mkoani humo na za ndani zinapandwa
miti kuanzia mikoa wanayopakana nayo kwa njia ya mstari ili kuweka
madhari mazuri na kuvutia watalii.
Alisema
kuwa wanataka kuhakikisha mgeni anapoingia katika Mkoa huo
anakaribishwa na miti iliyopandwa kwa wingi katika mistari iliyonyoka.
Mwanri
alisema kuwa zoezi linafanywa na wakazi wote wa Mkoa wa Tabora kuanzia
mashule hadi majumbani ili kujenga utamaduni wa eneo hilo kupenda miti
na kuacha tabia ya kukata ovyo.
0 comments:
Post a Comment